Aina mpya ya kirusi cha Covid-19 ambacho kimebadilika kabisa kilichopewa jina la Omicron kimeendelea kusambaa kote ulimwenguni, na kusababisha kufungwa mipaka na kurejeshwa hatua za kuzuia maambukizi.
Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema serikali zinahitaji kukielewa haraka kirusi hicho ambacho kiligundulika kwa mara ya kwanza kusini mwa Afrika.
Orodha ndefu ya nchi tayari zimeweka marufuku ya kusafiri kusini mwa Afrika, zikiwemo Qatar, Marekani, Uingereza, Indonesia, Saudi Arabia, Kuwait na Uholanzi.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametoa wito kwa nchi kuondoa marufuku za safari za ndege kabla ya uharibifu zaidi kutokea kwenya uchumi wa nchi zilizoathirika.
Uingereza, ambayo kwa sasa inashikilia uwenyekiti wa kundi la mataifa tajiri ya G7, imeitisha mkutano wa dharura leo kuujadili mzozo huo.