Meya wa Jiji la Dar es salaam, Isaya Mwita ameamua kwenda mahakamani kufuta kesi aliyoifungua ya kupinga kuondolewa madarakani kwakua haikuwa na mashiko tena.
Na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimtaka kuifuta kwa gharama kesi hiyo kwa madai kuwa wamepoteza muda, rasilimali na uandaaji wa majibu kuhusu shauri hilo.
Mwita amewasilisha maombi hayo kupitia Wakili wake Hekima Mwasipu mbele ya Hakimu Mkazi Janeth Mtega.
Wakili Mwasipu ameieleza mahakama kwamba miongoni mwa sababu zao ni kwamba anaona kesi hiyo haina maana kuwepo mahakamani kwa sababu hatua za kumng’oa madarakani zilishafanyika.
Pia muombaji (Mwita) hakupewa nafasi ya kusikilizwa mahakamani, hivyo anaomba kuliondoa shauri hilo bila gharama jambao ambalo Hakimu Mtega alikubaliana nalo ”“Nakubaliana na maombi ya muombaji (Mwita) ya kuliondoa shauri hili, hivyo naliondoa kwa gharama”.
Asubuhi ya leo Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isack Mwita alizuiwa kuingia katika ofisi yake na kukuta mlango wa Ofisi yake umebadilishwa nywila “Password” za kuingilia hali iliyolazimu kukaa nje kwa muda.
Akizungumza na Muungwana Blog kwa njia ya simu Mwita amesema mwanzo walimfungia mlango ila kwa sasa wamemfungulia na ameingia ofisini kufanya kazi zake za kila siku.
”Mimi bado ni meya na asubuhi ya leo nilivyofika katika ofisi yangu nikakuta mlango wa Ofisi yangu umebadilishwa Password za kuingilia nikaona hapa kutakuwa na kitu ila baada ya muda walishauriana na kunifungulia na nimeingia katika ofisi yangu na nikaamua kwenda mahakamani kwaajili ya kufuta kesi niliyoifungua awali” alisema Mwita.
Mwita alivuliwa umeya baada ya uamuzi wa kikao cha madiwani 16 wa chama tawala cha Mapinduzi, CCM, Meya Mwita alinyang’anywa gari alilokuwa akitumia na pia ofisi yake ya umeya kufungwa.
Baadhi ya hoja zilizotumiwa na madiwani wa CCM kumuondoa meya huyo wa upinzani ni pamoja na ile inayosema dereva wake alipata ajali kwa kutumia gari hiyo na pia mwenyewe alihusika na ubadhirifu wa takribani shilingi bilioni tano za umma mambo ambayo anayakana.