Hatua ya Shirika la Umeme ya kupandisha bei ya umeme bila kushirikisha mamlaka nyingine za Serikali, zimemgharimu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Felchesmi Mramba, ambaye jana amefutwa kazi na Rais John Magufuli.
Kabla ya kutengua uteuzi wa Mramba, Rais Magufuli ambaye jana alisali mjini Bukoba katika kanisa la Bikira Maria, Mama mwenye Huruma la mjini Bukoba, alisema Tanesco haikumshirikisha yeye, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Ewura juzi ilitangaza kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 8.5 baada ya Tanesco kuomba gharama zipande kwa asilimia 18.19, lakini hatua hiyo ilisitishwa na Profesa Muhongo.
“Waliopandisha umeme hawakuja kuniuliza hata mimi kiongozi wa nchi, hawakuuliza hata waziri mwenye dhamana, ya nishati hawakumuuliza hata Makamu wa Rais, Waziri Mkuu haiwezekani mtu akae pekee yake na afanye maamuzi yake pekee bila kushirikisha mamlaka nyingine,” alisema Rais.