Klabu ya Manchester United inataka kuwapa mshahara wa kibabe zaidi, Pauni 600,000 kwa juma washambuliaji Marcus Rashford na Harry Kane ili wawili hao wawe pacha hatari katika kuisogeza timu hiyo kwenye ubingwa wa Ligi Kuu England msimu ujao 2023/24.
Mpango huo wa Man Utd ni kutaka kutumia fursa ya kufanya vibaya kwa Tottenham ili kumnasa Mshambuliaji Kane, ambaye atahitaji kuwa na changamoto mpya.
Mlinda Lango David de Gea ndiye mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi Pauni 375,000 kwa juma klabuni hapo kwa sasa, lakini raia huyo wa Hispania mwenye umri wa miaka 32, mkataba wake utakwisha mwisho wa msimu huu na dili lake jipya litamuwezesha kulipwa mshahara wa Pauni 200,000 kwa juma.
Mshambuliaji Rashford mwenye umri wa miaka 25, atakuwa amebakiza miezi 12 zaidi kwenye mkataba wake na dili jipya litafanya mshahara wake upande kutoka Pauni 200,000 hadi Pauni 300,000 kwa juma.
Kane analipwa Pauni 200,000 kwa juma huko Spurs, lakini kama atatua Man United watamwongeza Pauni 100,000 na hivyo atakuwa analipwa Pauni 300,000 kwa juma.
Kane atafikisha umri wa miaka 30, Julai mwaka huu, lakini kuwa naye kwenye timu ni kujihakikishia mabao ya kutosha, hivyo kama atacheza pacha na Rashford kocha’ Erik ten Hag atakuwa na uhakika wa kikosi chake kuwa na fowadi ya kutisha.
Man United haijashinda ubingwa wa Ligi Kuu England tangu mwaka 2013, hivyo wanaamini kama watamchukua Kane kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi watakuwa kwenye nafasi kubwa ya kupambania ubingwa wa ligi hiyo msimu ujao.