Mtoto wa miaka saba, Lusambaja Bundala, mkazi wa wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, ameuawa na Baba yake mdogo kwa kupigwa kichwani na kitu chenye ncha kali kwa madai ya kupoteza ng’ombe aliokuwa akiwachunga.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Katavi, Benjamin Kuzaga, amesema tukio hilo lilitokea juzi saa nne asubuhi katika kitongoji cha Luhafwe, ambapo Juma Lusambaje (28), aliyekuwa akiishi na marehemu, alitekeleza mauaji hayo.

Kamanda Kuzaga ameeleza kuwa kabla ya kuuawa mtoto huyo alikuwa na mtoto mwenzake, Ibrahimu Lusambaja (13), na walitumwa kwenda kuchunga ng’ombe septemba 12.

Lakini tokea siku hiyo walipokwenda kuchunga ng’ombe, mtoto Bundala hakuonekana hadi juzi saa nne asubuhi alipokutwa amefariki dunia kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali kichwani na kuchomwa kisu chini ya kidevu.

Kamanda Kazuga ameeleza kuwa chanzo za mauaji hayo ni hasira za mtuhumiwa baada ya mtoto wake kupoteza ng’ombe aliokuwa anawachunga.

Amedai kuwa baada ya mtoto huyo kupoteza ng’ombe, mtuhumiwa alichukua sheria mkononi na kumpiga kwa kutumia chuma chenye ncha kali na kumchoma na kisu hadi umauti ulipo mpata.

Kamanda Kazuga amesema mtuhumiwa anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi na anatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazo mkabili.

Mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa mazishi baada ya kufanyiwa uchunguzi.

Ross Barkley ajitwisha mzigo wa lawama, Lampard amtetea
Adam Salamba kulipwa kwa dola