Na: Joseph Muhozi Josefly

Wakati Tanzania ikiwa kwenye majonzi mazito ya kuondokewa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliyekuwa Makamu wa Rais aliapishwa kushika nafasi hiyo kwa mujibu wa Katiba, akiwa Rais wa kwanza mwanamke Tanzania.

Unaweza kusikiliza makala hii kwa kubofya hapa:

Rais Samia ameanza kuwahakikishia Watanzania kuwa alifundishwa vizuri na Hayati Dkt. Magufuli, na sasa yeye ndiye Rais na hakuna jambo litakaloharibika eti kwa sababu ni mwanamke. Hivyo, kwa wenye mashaka waondoe shaka.

Jana, Machi 28, 2021 Rais Samia ameanza kwa kishindo cha aina yake alipokuwa akipokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Sauti yake nzuri ya upole na ustaarabu imeonesha kuwa na Mamlaka ya vitendo, hasa baada ya kumsimamisha Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari, Mhandisi Deusdedit Kakoko, kuagiza uchunguzi wa fedha zote zilizolewa Benki Kuu kuanzia Januari hadi Machi, 2021 na kumpa kumpa nafasi ya mwisho Waziri wa TAMISEMI, Selemani Jafo kushughulikia suala la mapato na matumizi ya taasisi za wizara hiyo.

Maagizo kwa Waziri Jafo yakaibua k auli iliyokuwa gumzo (trending) mitandaoni, “ukishindwa tuambie tukusaidie.”

Kishindo cha kwanza cha Rais Samia, ambacho waingereza wanasema ‘Madam President landed running’, kwa tafsiri isiyo rasmi ni kwamba ‘Rais ametua akiwa kwenye mwendo’. Kishindo hicho kimewavutia wengi akiwemo aliyekuwa Mbunge wa Mikumi kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joseph Haule, ambaye pia ni nguli wa muziki maarufu kama Profesa Jay’.  Yeye amemtaka mwanaye wa kike kusoma kwa bidii ili kesho yake iwe ng’aavu kama ya Rais Samia.

Ingawa kuna zaidi ya wanawake 70 waliowahi kufanya kazi nzuri na kuzineemesha nchi zao waliposhika madaraka katika dunia ya sasa. Leo nitakueleza habari ya wanawake sita waliovunja rekodi ya dunia baada ya kuchaguliwa kuongoza nchi katika nafasi za juu zaidi wakiongoza Serikali na wakafanya kazi kubwa iliyoandika historia katika dunia ya sasa. Kama nitamtaja kama Waziri Mkuu, basi katika mfumo wa nchi hiyo, Waziri Mkuu ndiye Kiongozi wa Serikali.

6. Sirimavo Bandaranaike – Sri Lanka

Sirimavo Bandaranaike, alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu wa Sri Lanka mwaka 1960, wakati huo ikifahamika kama Ceylon. Huyu ndiye mwanamke wa kwanza duniani kuchaguliwa kuwa Kiongozi Mkuu wa Serikali katika dunia ya sasa (modern world).

Mwanamke huyu shupavu aliukataa unyonge na kukatishwa tamaa. Alianzia kwenye maumivu makali, akakaza moyo na kufunga bandage kwenye kidonda cha moyo, kisha akauchapa mwendo hadi kushika kuvunja rekodi. Ni hivi, Mama Bandaranaike aliamua kuingia kwenye siasa baada ya mume wake aliyekuwa Waziri Mkuu kuuawa kwa chuki za kisiasa.

Sirimavo Bandaranaike – Sri Lanka

 Baada ya kifo cha mumewe, alifanikiwa kushika jembe na kuwa kiongozi wa chama kilichoongozwa na mumewe cha Freedom Party. Aliongoza taifa lake kama Waziri Mkuu tangu mwaka 1960-1965, na baadaye akachaguliwa tena kuwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 1970-1977. Anakumbukwa kwa kuwa kiongozi shupavu aliyeanzisha mfumo bora wa biashara zinazofaidisha wanyonge, Serikali ikasuka mfumo bora wa biashara. Maji hufuata mkondo, akampika binti yake aitwaye Chandrika Kumaratunga. Chandrika akafanikiwa kuwa Rais wa kwanza wa Sri Lanka mwanamke aliyeongoza taifa hilo kuanzia Mwaka 1994-2005.

5. Indira Gandhi – India

Indira Gandhi aliandika historia ya kuwa Mwanamke wa kwanza kuwa Waziri Mkuu wa India, na hadi leo hakuna mwanamke mwingine aliyewahi kushika wadhifa huo.

Huyu ni mwanamke wa chuma aliyeacha alama kubwa ya uongozi katika dunia hii. Alizaliwa Novemba 19, 1917. Alithibitisha kuwa mtoto wa nyoka anaweza kuwa zaidi ya nyoka. Indira Gandhi alikuwa mtoto wa mwanaharakati na Waziri Mkuu wa India, Jawaharlal Nehru.

Mwanamke huyu wa shoka alianza kung’ara baada ya kujiunga kwenye harakati za kutafuta uhuru wa India akiwa msichana mdogo. Kutokana na uwezo wake alipata umaarufu mkubwa. Mwaka 1966 alichaguliwa kuongoza chama cha Congress Party, na alikuwa Waziri Mkuu wa India kuanzia Januari 1966 hadi Machi 1977. Uchaguzi uliofuata alishindwa, akakubali matokeo. Akarejea tena ulingoni mwaka 1980 na akashinda tena kuwa Waziri Mkuu, kwa sababu kazi yake ilionekana ni kubwa kuliko aliyemuachia ofisi.

Indira Gandi aliuawa na walinzi wake mwenyewe mwaka 1984, kutokana na mvutano wa siasa zilizogusa masuala ya imani.

Rais wa zamani wa India, Pranab Mukherjee anasema Indira Gandi ni Waziri Mkuu bora kuwahi kutokea nchini humo, na kwamba alikuwa mkweli kama Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, kwake nyeusi ilikuwa nyeusi na nyeupe ni nyeupe.

4. Golda Meir – Israel

Alizaliwa Ukraine mwaka 1898, lakini aliitawala Israel kama Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke katika taifa hilo, na kwenye historia ya dunia ya sasa alikuwa mwanamke wa tatu kushika nafasi hiyo duniani. Alipiga kazi kubwa kwa kipindi cha miaka 40 ndani ya Israel, akisaidia mapambano ya Israel kujipatia uhuru na kuwa Taifa huru, hadi mwaka 1969 alipochaguliwa kuwa Waziri Mkuu.

Maisha yake yalikuwa ya mapambano. Utajiuliza, ilikuwaje mzaliwa wa Ukraine akaitawala Israel. Bi. Golda Meir, aliishi uhamishoni mara kadhaa. Alizaliwa Ukraine, akahamia Marekani na kuishi huko utotoni. Alijiunga na mapambano ya kuliunda taifa huru la Israel, akapata nafasi ya kuwa msemaji mkuu wa Zionist wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Matokeo ya mapambano yake, yalimfanya kuwa kati ya wanawake wawili pekee walioshiriki mchakato wa kutia Saini tamko la uhuru wa Israel, la mwaka 1948.

Golda Meir

Kama mama, alipenda amani, na aliisimamia hadi ikamuondoa ofisini. Akiwa Waziri Mkuu alianzisha mazungumzo ya kusaka amani kati ya Israel na mataifa ya Jirani. Lakini harakati zake za amani ziliingiwa na shetani, baada ya kutokea vita kubwa mwaka Oktoba 1973. Vita hiyo ni maarufu sana inaitwa ‘Yom Kippur War’ au ‘Oktoba War’. Ambapo, nchi za umoja wa Kiarabu zilijipanga kuipiga Israel kwa kushtukiza, wakati Mama akiwa anaendelea kutafuta amani kati yao. Nchi hizo ziliongozwa na Misri na Syria. Mwaka 1974, aliamua kujiuzulu nafasi ya Uwaziri Mkuu baada ya alichokuwa anakipigania, yaani amani kuingia doa. Alifariki miaka minne baadaye baada ya kuugua saratani ya lymphoma

3. Margaret Thatcher – Uingereza

Bi. Margaret Thatcher, aliyefahamika pia kama mwanamke wa Chuma, alikuwa mkemia kama Hayati Dkt. John Magufuli. Bi. Thatcher alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, akiweka rekodi pia ya kuwa Waziri Mkuu aliyetawala kwa muda mrefu zaidi Uingereza katika karne ya 20. Aliitawala Uingereza kuanzia mwaka 1979-1990.

Ndani ya kipindi cha miezi sita tu tangu alipoingia madarakani, alifanya mageuzi makubwa Uingereza. Maisha yakawa matamu ghafla. Kazi yake nzuri ilimpa nafasi ya kukalia kiti hicho kwa miaka 11 na kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza aliyekaa madarakani kwa muda mrefu zaidi katika karne ya 20 na kufanya makubwa.

Margaret Thatcher

2. Angela Merkel – Germany

Huyu pia ni Mkemia, ana Shahada ya Uzamivu (PhD) ya Kemia kama Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Aliingia kwenye michakato ya siasa punde baada ya kuanguka kwa ukuta wa Berlin (Berlin Wall) Novemba 9, 1989.

Bi. Angela Merkel, aliweka rekodi ya kuwa Mwanamke wa kwanza kuwa Chancellor wa Ujerumani, taifa linaloshika nafasi ya nne kwa nguvu ya uchumi duniani. Lakini sio tu kwamba alikuwa mwanamke wa kwanza, aliweka rekodi pia ya kuwa mtu mwenye umri mdogo zaidi kushika nafasi hiyo akiwa na umri wa miaka 51. Safari yake ya juu ya uongozi ilianzia mwaka 2000 alipokiongoza chama cha Christian Demorratic Union. Miaka mitano baadaye akawa Chancellor wa Ujerumani, kiti ambacho amekikalia hadi leo ambapo ana umri wa miaka 66.

Angela Merke

Markel ni mama na jembe kwelikweli. Amekuwa akitajwa kuwa ndiye mwanamke mwenye nguvu zaidi duniani kwa sasa, hii inamaanisha nguvu ya kimfumo. Katika kipindi chake, Ujerumani imepanda kwa kasi. Alifanikiwa kupunguza tatizo la ajira kwa zaidi ya asilimia 50, akapandisha mapato ya Serikali kwa kasi hadi kuvuka makadirio. Wakati wa mzozo wa mwaka 2015 kuwapokea au kutowapokea wakimbizi nchini humo, Markel aliamua kama mama na kiongozi, Ujerumani ikawapokea maelfu ya wakimbizi kutoka Syria na nchi jirani.

  1. Ellen Johnson Sirleaf – Liberia

Huyu ni mwanamke wa chuma aliyefungua dirisha la baraka kwa wanawake Afrika. Alikuwa Rais wa 24 wa Liberia, lakini mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo, akihudumu kuanzia mwaka Januari 16, mwaka 2006 hadi Januari 22, mwaka 2018.  Bi. Sirleaf ambaye hivi sasa ana umri wa miaka 82, alizaliwa Oktoba 29, 1938.

Kabla ya kushika nafasi ya urais, aliyapitia mengi hadi kuwa Waziri wa Fedha. Aliwahi kufanya kazi benki. Uwezo wake ukampandisha hadi kuwa Waziri wa Fedha. Lakini alishakwepa mishale kadhaa iliyompa nguvu na ukomavu. Kutokana na changamoto ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, aliwahi kulazimika kukimbilia uhamishoni. Alikimbilia Kenya akapewa hifadhi kwa kuwa Afrika ni moja.

Mwaka 2005, Bi. Sirleaf alishinda kwa kishindo uchaguziwa wa urais, akipata zaidi ya asilimia 80 ya kura zote, akawamwaga wagombea wote wanaume.

Katika kipindi cha miaka 12 ya utawala wake, Bi. Sirleaf alifanikiwa kurejesha amani ya kudumu katika taifa hilo, na vita ikawa historia. Pia, alifanikiwa kuwashawishi mataifa yanayoidai Liberia, kuifutia deni la takribani $5 bilioni. Liberia ikawa haina deni hilo la Taifa. Alifanikiwa pia kuisaidia nchi hiyo kupambana na ugonjwa hatari wa Ebola. Akalilea taifa hilo kama mama.

Ellen Johnson Sirle

Kwa kazi nzuri na kubwa aliyoifanya, mwaka 2011 dunia ilimtunukia Tuzo ya Amani ya Nobel.

Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyekuwa Makamu wa Rais lakini Watanzania tumemuita ‘Mama wa Taifa.’ Tunaamini atatulea vizuri kama mama na kama kiongozi wetu, tutavuka. Dar24 Media tunaungana na Watanzania kumuombea kwa Mwenyezi Mungu.

Waziri Mkuu wa Armenia ajiuzulu
ACT Wazalendo yashinda Pandani, CCM yashinda Kununi Unguja