Kiungo Mshambuliaji kutoka DR Congo na klabu ya RS Berkane ya Morocco Tuisila Kisinda amesema wanatarajia upinzani mkubwa kutoka kwa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC.
Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo wa ‘Kundi D’, Kombe la Shirikisho Barani Afrika utakaopigwa Jumapili (Machi 13), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Tuisila Kisinda ambaye aliwahi kuitumikia Young Africans kabla ya kutimkia Morocco mwanzoni mwa msimu huu 2021/22, amesema wamejiandaa kupambana bila kuchoka, huku akisistiza wanawaheshimu Simba SC.
Amesema kila mmoja kwenye kikosi chao anafahamu Uwanja wa Benjamin Mkapa ni sehemu ngumu kupata ushindi hasa unapokutana na Simba SC kwenye michuano ya Kimataifa, hivyo wamejizatiti kukabiliana na hali hiyo.
“Tunafahamu mchezo wa Jumapili, utakuwa mgumu pengine zaidi ya ilivyokuwa Morocco, lakini tutapambana ili tutimize lengo la kuondoka na alama tatu.”
“Tunajua Simba SC wamejiandaa na watahitaji kulipa kisasi cha kupoteza mchezo uliopita dhidi yetu, pia Uwanja wa Mkapa ni mahala ambapo wanapaamini sana kupata matokeo mazuri, lakini hata sisi tumekuja kwa ajili ya kupambana na kushinda.” amesema Kisinda
Simba SC ilipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya RS Berkane katika mchezo wa Mzunguuko wa tatu wa Kundi D, Februari 27 mjini Berkane-Morocco hivyo itahitaji kulipa kisasi kwa kusaka ushindi ili kurejea kileleni mwa msimamo wa Kundi hilo.
Kabla ya mchezo huo Simba SC ilikua inaongoza msimamo wa Kundi D kwa kuwa na alama 04, huku Berkane iliyopoteza mchezo wa Mzunguuko wa pili dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast ilikua na alama 03.
Hadi sasa Msimamo wa Kundi D, unaonyesha kuwa RS Berkane inaongoza ikiwa na alama 06, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama o4 sawa na USGN ya Niger huku ASEC Mimosas ya Ivory Coast ikiburuza mkia ikiwa na alama 03.