Mlinda Lango wa Mtibwa Sugar Jeremiah Kisubi hatopata nafasi ya kucheza dhidi ya Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, siku ya Jumamosi (Januari 22).
Imethibitishwa kuwa Mlinda Lango huyo aliyesajiliwa kwa mkopo huko Manungu Complex akitokea Simba SC, hatokua kwenye kikosi cha Mtibwa Sugar, kufuatia mkataba wake kutompa nafasi ya kuwa sehemu ya mchezo huo.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Simba SC Ahmed Ally amesema Mkataba wa mkopo wa Kisubi wakati akijiunga na Mtibwa Sugar, una kipengele cha kumzuia kucheza dhidi ya waajiri wake, ambao walimsajili mwanzoni mwa msimu huu akitokea Tanzania Prisons.
“Mkataba wa Kisubi nimeuona, una kipengele kinachomzuia kutocheza dhidi ya Simba SC, na hii imekua ni kawaida sana kwa wachezaji kama hawa ambao hutolewa wa mkopo kwenye klabu zinazocheza ligi moja.”
“Said Ndemla, Ibrahim Ame wao watacheza mchezo wetu dhidi ya Mtibwa Sugar, kwa sababu mikataba yao haiwanyimi nafasi ya kucheza dhidi ya klabu ya Simba SC.” amesema Ahmed Ally akiwa kwenye kipindi cha Sports Arena cha Wasafi FM
Simba SC itacheza mchezo wake dhidi ya Mtibwa Sugar, katika Uwanja wa Manungu Complex, ikiwa ni mara ya kwanza kwa klabu hizo kukutana uwanjani hapo, baada ya miaka 21.
Mara ya mwisho Simba SC ilikutana na Mtibwa Sugar Manungu Complex mwaka 2000, na mchezo huo haukuisha kufuatia kikosi cha Simba SC kugomea mchezo.