Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali umeridhia na kupitisha ombi la Tanzania la kutaka Kiswahili kuwa lugha ya kazi katika Umoja huo.
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango aliwasilisha ombi hilo la lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha za kazi katika mikutano ya Umoja wa Afrika, kwani lugha hiyo ni miongoni mwa lugha za kiafrika zenye wazungumzaji wengi barani Afrika ambapo takribani watu milioni mia moja wanakitumia Kiswahili pamoja na wazungumzaji kutoka nje ya Bara la Afrika.
Kutokana na umuhimu wa lugha hiyo Makamu wa Rais amesema tayari inatumika katika jumuiya mbalimbali ikiwemo jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) pamoja na kufundishwa kwa lugha hiyo katika nchi nyingi za Afrika Mashuleni.
Amesema tayari Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni limetangaza tarehe saba Julai ya kila mwaka kuwa siku ya maadhimisho ya lugha Kiswahili Duniani.
Mkutano huo pia umeichagua Tanzania kuwa mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (AU)
Pamoja na mambo mengine mkutano huo wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja Afrika (AU) nchi wanchama zimelaani vitendo vya uvunjaji katiba uliopelekea mapinduzi ya kijeshi katika mataifa mbalimbali pamoja na vitendo vya ugaidi vinavyoendelea katika mataifa mbalimbali barani Afrika. Umoja wa Afrika umeasa majadiliano kuendelea katika nchi hizo ili kurejesha utawala wa kiraia na kidemokrasia.
Katika kupambana na Uviko19, Umoja wa Afrika umetoa rai kwa nchi kushirikiana katika kukabiliana na janga hilo ikiwemo kuhakikisha chanjo zinapatikana pamoja na kuyaunga mkono mataifa yalioanza jitihada za kuzalisha chanjo hiyo barani Afrika ikiwemo Afrika Kusini, Senagal na Rwanda.