Mabingwa wa soka nchini Italia Juventus FC wanakaribia kukamilisha usajili wa mshambuliaji kutoka Ureno na klabu ya Real Madrid ya Hispania Cristiano Ronaldo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na kituo cha televisheni cha Sky Sports cha England, mpango wa uhamisho wa mshambuliaji huyo unatajwa huenda ukakamilika ndani ya saa 48 zijazo, kufuatia uongozi wa Juventus FC kukubali ada ya pauni milioni 88.
Sky Sports wamebainisha kuwa, pamoja na ada hiyo kukubaliwa, bado maungumzo kati yapande hizo mbili yanaendelea, hususan katika upande wa makubaliano binafsi kati ya mchezaji na uongozi wa Juventus.
Katika mazungumzo hayo Ronaldo anawakilishwa na wakala wake wa siku nyingi Jorge Mendes.
Mendes amewahi kuzungumza na baadhi ya vyombo vya habari na kueleza kuwa, endapo mchezaji wake atakamilisha hatua ya kuondoka Real Madrid na kwenda mahala pengine kucheza soka lake, atakua mwenye furaha mpya, kutokana na kuamini muda wa kufanya hivyo ni sasa.
“Endapo jambo hilo litakamilishwa kama tunavyotarajiwa, Ronaldo atakua na shauku ya kucheza soka kwa juhudi zaidi tofauti na ilivyokua Real Madrid, amenihakikishia hilo, kwa sababu anaamini anahitaji changamoto mpya katika maisha yake ya soka,” alisema Mendes alipohojiwa na vyombo vya habari vya Ureno.
“Ninaamini kila kitu kitawezekana na kitakamilishwa kwa wakati, mpaka sasa tunaendelea vyema na hata Cristiano Ronaldo anaonyesha kufurahia taratibu zilipofikia hadi sasa.” Ameongoza wakala huyo maarufu duniani.
Ronaldo, ambaye ni mfungaji bora wa muda wote kwenye klabu ya Real Madrid, anatarajiwa kuondoka klabuni hapo baada ya kuweka rekodi ya kufunga mabao 450, kutwaa mataji mawili ya ligi ya nchini Hispania, mataji mawili ya kombe la mfalme (Copa del Reys) na mataji manne ya ligi ya mabinbgwa barani Ulaya.