Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema Taasisi ya Jiolojia na Ufafiti wa Madini Tanzania – GST, ndiyo Moyo wa Sekta ya Madini na inategemewa na Wizara ya Madini na Sekta ambata ikiwemo ya Maji, Kilimo na Ujenzi.
Mavunde ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa GST jijini Dodoma ikiwa ni kikao chake cha kwanza baada ya kukabidhiwa ofisi na mtangulizi wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko.
Amesema, “GST ni kinara wa utoaji wa taarifa za masuala ya Jiolojia Barani Afrika hivyo hakikisheni mnaweka mikakati ya kufanya taasisi hii iwe bora zaidi katika sekta ya madini, inafanya tafiti mbalimbali kugundua migodi ya wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo tutaipa kipaumbele.”
Aidha, Mavunde pia ameitaka GST kutengeneza mashirikiano na taasisi zingine za utafiti wa Madini duniani kwa lengo la kupata uzoefu, ujuzi na uwezo wa taasisi wa kupata vifaa vya kisasa zaidi na kuwa na Maabara bora Barani Afrika na kuifanya taasisi hiyo kuwa sehemu ya utambulisho wa Tanzania.