Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza Wataalamu wa mifumo na TEHAMA, kubuni programu tumizi ya kuweza kutambua risiti halali na zisizo halali, ili kujihakikishia kuwa mapato yote yanayokusanywa yanaingia Serikalini.

Majaliwa ameyasema hayo hii leo Septemba 8, 2023 wakati wa kuahirisha Mkutano Wa 12 wa Bunge jijini Dodoma huku akiwataka waweke utaratibu wa kufanya kaguzi za mashine za “PoS” ili kubaini kama kuna ukiukwaji wowote unaofanyika sambamba na kuwa na utaratibu endelevu wa ufuatiliaji na mfumo wa usalama maalum wa utunzaji taarifa.

Amesema, “niwakumbushe watumishi wa umma bado tuna jukumu la kuendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato kama Rais Samia alivyosisitiza juu ya usimamizi wa ukusanyaji mapato kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa wakati akifunga mafunzo ya Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa mjini Kibaha.”

Aidha, Majaliwa amesema Serikali iliunda mfumo mpya wa ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri ujulikanao kama TAUSI, ili kupunguza urasimu uliokuwepo kwenye ukusanyaji wa mapato na kudai kuwa mfumo huo mpya ni wa kidijitali na humrahisishia mfanyabiashara kufanya malipo kwa njia ya mtandao.

“Mfumo huu umelenga kumsaidia mteja kujihudumia mwenyewe, hali ambayo haimlazimu tena kwenda ofisi za halmashauri kuomba au kulipia tozo, ushuru, leseni, faini au vibali mbalimbali. Badala yake anaweza kufanya mwenyewe kupitia dirisha la mteja au Taxpayer Portal,” amesema Majaliwa.

Hata hivyo, amessisitiza kuwa, “Wafanyabiashara na watoa huduma watoe risiti halali kupitia mashine za kielektroniki (EFDs) wakati wa mauziano ya bidhaa au utoaji wa huduma kwa wateja. Kwa upande wa wateja, niwakumbushe kuwa ni wajibu wao kudai risiti yenye thamani halisi ya fedha walizotoa.”

Ronaldo: Ushindani wangu na Messi umekwisha
Matumaini kibao kwa kocha Middendorp