Baada ya kuianza Ligi Kuu kwa aibu kwa kutinga uwanjani na kikosi chenye wachezaji pungufu, Kitayosce sasa imejipata na imeipiga mkwara Singida Fountain Gate kwamba wakutane Uwanja wa Liti, Singida wawaonyeshe kazi.
Kitayosce iliyopanda Ligi Kuu kwa mara ya kwanza ikiwa sambamba na JKT Tanzania na Mashujaa FC, iliishia kuchapwa mabao 4-0 na Azam FC katika mechi iliyochezwa kwa dakika 15 tu kabla ya kumalizwa na kutokana na kuwa na wachezaji pungufu ikianza na wanane na kumalizia na sita.
Timu hiyo inarudi uwanjani Alhamisi (Septemba Mosi) kuvaana na Singida na nahodha Saidy Mbaty amesema mchezo huo ujao ndio wataanza kuonyesha uwezo wao halisi, ubora wa kikosi hicho na dhamira ya ushiriki katika Ligi Kuu msimu huu kwa vile wameshasahau kilichotokea dhidi ya Azam FC.
Ikiwa imeweka kambi ya juma moja mkoani Morogoro ikijifua vikali chini ya kocha Goran Kopunovic kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Singida, Mbatty aliyepanda na timu hiyo amesema baada ya kile kilichotokea Chamazi wamekaa chini na kuzungumza na kukubaliana kutazama zaidi mbele katika michezo inayofuata ili kuwapa furaha mashabiki huku akiahidi msimu huu watafanya vizuri na kuwapa raha.
“Maandalizi yako vizuri na morali kwa wachezaji iko juu hatuangalii kilichopita, tunazingatia zaidi mchezo unaofuata, tunajitoa kwa ari na kila mtu ana morali kwa ajili ya kuonyesha kile kitu ambacho Tabora United inahitaji kwenye mechi inayofuata” amesema Mbaty, huku kocha Goran ambaye hakuwepo kwenye mchezo wa kwanza, akisisitiza malengo yao msimu huu ni kutoshuka daraja.
“Tuna furaha kwenye timu tunaendelea na maandalizi, mimi sio mtu wa mazingaombwe wala kutoa ahadi, ninachoweza kusema kwa sasa tunapambana kadri ya uwezo wetu kila siku tunatafuta kitu kizuri na kuvuna pointi kila mchezo,” amesema Goran aliyewahi kuinoa Simba SC.