Maombi ya Kesi ya aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu kupitia kwa wakili wake dhidi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai inatarajiwa kuanza kusikilizwa leo katika mahakama kuu ya Tanzania masjala kuu ya Dar es salaam.
Katika kesi hiyo, Lissu anapinga uamuzi wa spika Job Ndugai wa juni 28 mwaka huu wa kumvua ubunge wa jimbo la Singida Mashariki.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Chadema, Tumaini Makene imesema kuwa maombi hayo yatasikilizwa mbele ya Jaji Mtupa.
Aidha, taarifa hiyo ya Makene imesema kuwa hati ya wito wa mahakama inabainisha kuwa mlalamikiwa ambaye ni Spika wa bunge, Job Ndugai atalazimika kufika mahakamani hapo bila kukosa akiwa na nyaraka zote.
”Tunatoa wito kwa viongozi, wanachama, wafuasi wa Chadema na Watanzania wote wapenda haki, demokrasia na utawala bora unaoheshimu sheria, mahali popote walipo kufuatilia kwa karibu shauri hili kuanzia sasa,”imesema taarifa hiyo iliyotolewa na Makene
Hata hivyo, katika taarifa hyo, ameeleza kuwa wameamua kutafuta haki mahakamani baada ya spika Ndugai kutangaza kukoma kwa Ubunge wa Lissu juni 28 mwaka huu alipokuwa akiahirisha mkutano wa Bunge la Bajeti jijini Dodoma.