Rais wa Bunge Bärbel Bas ametangaza rasmi matokeo baada ya bunge leo Disemba 8, 2021 kupiga kura ya siri kumuidhinisha Scholz kuwa kansela mpya wa Ujerumani, ambaye alikuwa naibu kansela na Waziri wa fedha katika serikali ya muungano.

Olaf Scholz amechukua mikoba ya Angela Merkel na kuwa Kansela mpya wa Ujerumani baada ya kushinda kura 395 kati ya kura 707 zilizopigwa bungeni kumuidhinisha katika nafasi hiyo.

Chama chake cha SPD na washirika wake wawili, chama cha walinzi wa mazingira Die Grüne au chama cha kijani na kile cha FDP wana takriban viti 416 katika bunge jipya la Ujerumani hali iliyotoa ishara ya mapema kwamba angelishinda nafasi hiyo ya kuwa kansela.

Baada ya kuidhinishwa, Sholz na Baraza lake la mawaziri  lililo na wanachama 16, saba kutoka chama cha SPD watano kutoka chama cha kijani na wanne kutoka chama cha FDP wanatarajiwa kuthibitishwa na rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier  kabla ya kuapishwa bungeni.

Baadaye mawaziri waliohudumu katika serikali ya Merkel pia watapewa nafasi hii leo kukabidhi madaraka kwa mawaziri wapya. Scholz, aliyehudumu kama waziri wa fedha atamkabidhi majukumu hayo ya kifedha kiongozi wa FDP Christian Lindner.

Serikali ya Scholz inaingia madarakani ikiwa na matumaini makubwa ya kuifanya Ujerumani kuwa ya kisasa zaidi kwa kukumbatia mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi huku ikikumbwa na chamgamoto kubwa zaidi ya kukabiliana na janga la COVID 19.

Tafsiri halisi ya Disemba 9 kimaendeleo
Makubaliano ya Biden na Putin hayafikia muafaka