Scolastica Msewa, Chalinze – Pwani.
Ujenzi wa kituo Cha kupoza umeme cha Chalinze na mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Julias Nyerere JNHPP hadi Chalinze utekelezaji wake wa jumla umefikia asilimia 86.23 ambapo Desemba 31, 2023 Umeme unatarajiwa kuwashwa licha ya mvua zinazoendelea kunyesha nchini kote kukwamisha kazi hiyo.
Hayo yamebainika wakati ikitolewa taarifa kwa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Pwani, iliyofika kukagua Maendeleo ya Ujenzi wa Kituo cha kupoza Umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Julias Nyerere kuja Chalinze wakati wakiwa katika siku nne ya ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM Mkoa wa Pwani.
Kaimu Meneja Mradi, Eng. Fillipo Faraja Maliwa amesema kukamilika kwa kituo hicho kitaboresha upatikanaji wa umeme kwenye Gridi ya Taifa na kuongeza hali ya ubora na uhakika wa upatikanaji wa umeme katika Gridi ya Taifa kwa kuunganisha umeme wa JNHPP kupitia kituo hicho cha kupoza umeme cha Chalinze.
Alisema ujenzi huo kwa upande wa usanifu umefikia asilimia 91.78 na usimikaji wa mitambo umefikia asilimia 81.18 huku ununuzi wa vifaa ukifanyika kwa asilimia 97.83 na majaribio ya ufanisi yakifikia asilimia 29.47 ambapo mpaka sasa zaidi asilimia 95 ya vifaa vyote vimeshawsili nchini ambapo Mradi huo unagharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia 100.
Gharama za mradi huo mpaka kukamilika ni shilingi bilioni 128 ambapo shilingi bilioni 57.9 sawa na aslimia 54.2 zimelipwa hadi mwezi Novemba huku Injinia Maliwa akisema mvua zinazoendelea kunyesha zinakwamisha utekelezai wa ujenzi wa mradi huo ingawa wanajitahidi kuendelea na kazi.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Mwinshehe Mlao mbali na kumshukuru Rais pia amesema, “tuna matumaini nanyi sana kwamba ikifika mwezi Desemba 31 matumaini yetu ni kuona umeme haukatiki tena nchini kuanzia siku hiyo. Tumeona mitambo, tumeona kazi iliyofanyika na tumeona wafanyakazi tunawashukuru sana.”
Amesema fedha hizo zimeleta suluhisho la changamoto zilizokuwa zikiikabili huduma ya afya katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo na kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule za Msingi Kiharaka na Bwilingu ambapo zimepatikana shule mbili mpya kupitia mradi wa BOOST.
Aidha aliwapongeza Wabunge wa Majimbo ya Bagamoy, Muhalami Mkenge, wa Chalinze Ridhiwani Kikwete, Wakurugenzi na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo kwa usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo huku akiwataka watumishi wa Halmashauri zote mbili kuendelea kuwa waaminifu na waadilifu kwa kutunza kile kinachopatikana kupitia mapato ya ndani.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Kamati hiyo ya Siasa ilikagua miradi miwili ikiwa ni pamoja kutembelea Ujenzi wa Shule mpya ya awali na Msingi Kiembeni, ambayo imejengwa kwa fedha za mradi wa Boost na kusaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule ya msingi Kihalaka yenye Wanafunzi zaidi ya 900 waliohamishiwa katika shule hiyo.