Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Wilaya za Temeke na Mkuranga kuangalia namna ya kupunguza msongamano uliopo katika eneo la Mbagala.

Majaliwa amesema hayo leo Februari 7, 2017 alipokutana na viongozi wa wilaya hizo Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutafua njia za kuondoa msongamano huo, na moja ya hatua alizowashauri kuchukua ni pamoja na kuhamisha kituo cha mabasi ya mikoa ya kusini ya Lindi, Mtwara na Ruvuma kutoka Temeke hadi Mkuranga..

Amesema kwa sasa hakuna namna ambayo wataweza kuondoa msongamano huo zaidi ya kuhamishia kituo cha mabasi ya mikoa ya kusini wilayani Mkuranga, amesema eneo la Mbagala kwa sasa lina msongamano mkubwa ambao ni lazima Serikali ichukue hatua za haraka za kuuondoa.

“Ikiwezekana mabasi ya mikoa ya kusini yaishie Mkuranga, hivyo shirikianeni kutafuta eneo la kujenga kituo kikubwa cha kisasa cha mabasi,” amesema.

Majaliwa amesema kituo hicho watakachokijenga kiwe na uwezo wa kuhudumia mabasi yote yatokayo mikoa ya kusini na kituo cha Mbagala kiwe cha daladala za kawaida.

Pia amesema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa kituo hicho kutawezesha kuongeza mapato ya Halmashauri ya wilaya ya Mkuranga.

Majaliwa amewataka viongozi hao kwenda kujadiliana katika vikao vya mabaraza ya Madiwani juu ya mkakati huo na kisha kumpelekea taarifa ifikapo Februari 15 mwaka huu.

Akizungumza Mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Filberto Sanga amesema wazo hilo ni zuri na wilaya yake ina maeneo ya kutosha kujenga miundombinu hiyo.

“Ni kweli wilaya ya Temeke imeelemewa kwa maana ya maeneo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maendeleo na haina pa kupumulia zaidi ya Mkuranga , hivyo tupo tayari kushirikiana nao,” amesema.

Aidha, Sanga ameiomba Serikali itakapoanza awamu ya tatu ya ujenzi wa mradi wa mabasi ya mwendo kasi ufike hadi Mkuranga mjini badala ya kuishia Vikindu.

Amesema kwa sasa wilaya yake ina viwanda 67 ambavyo kati yake vipo vinavyofanya kazi na vingine vikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi, hivyo mabasi hayo yatarahisisha usafiri kwa wafanyakazi.

El-Hadj Diouf Awatumia Ujumbe Waliogoma
Serikali kudhibiti matumizi holela ya fedha za kigeni