Serikali ya Tanzania itatumia bilioni 7 kujenga kituo maalumu cha kutolea huduma ya magonjwa ya mlipuko kitakachokuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 200
Katibu mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Zainabu Chaula amesema kituo hicho kitakapo kamilika kitatumika kulaza wagonjwa na washukiwa wa magonjwa ya milipuko ikiwemo Corona.
”Serikali imeamua kujenga kituo hicho kitakacho gharimu bilioni 7 na kitakapo kamilika kitakuwa cha aina yake nchini kwani kitawekwa vifaa vya kisasa vya kurahisisha utoaji wa huduma kwa wagonjwa wa magonjwa ya mlipuko” amesema Dk Chaula.
Akizungumza na makatibu wakuu na wajumbe wa kamati ya kitaifa ya kupambana na virusi vya Corona meneja wa mradi wa kituo hicho Kanali Solomoni Shaushi amesema baadhi ya majengo yatakamilika April 30,2020.
Aidha amesema kuwa ujenzi huo utafanywa na kikosi cha ujenzi cha Suma JKT na tayari Jeshi limeshapeleka kikosi kazi cha wanajeshi 389 kukamilisha ujenzi wa majengo yote baada ya mieziĀ sita.