Mwanasiasa na aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya ndani, Charles Kitwanga amemshukia Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kwa kusema ameshindwa kuwa na mipango thabiti ya kumkomboa Mkulima na kuwakomboa Watanzania kiujumla kwani harakati zake nyingi kiutendaji hazina matumaini.
Kitwanga ameyasema hayo wakati akifanya mahojiano na Dar24 Media na kuongeza kuwa Mkulima na Mtanzania wamekuwa hawafaidiki na uwepo wa fursa mbalimbali za sekta ya Kilimo zilizopo nchini kutokana na walioshika mamlaka kuwa na maono hafifu au kutojua njia za kupita ili kuleta nafuu ya gharama za maisha kwa jamii.
Amesema, “Bashe ni mzuri sana wa kuwadanganya wananchi alielezea namna ya kuwasaidia vijana kupata ajira bilioni 3 na kuna vijana 16,000 ili wafanye kilimo hiyo inasaidia nchi? nchi za uarabuni zinachukua maji baharini zinayachuja zinafanya kilimo na kilimo cvhenyewe ni kwa ajili ya kutengeneza mali ghafi itakayotengeneza mikate ambayo ni kilimo cha ngano.”
“Hivi kama watu wanachukua hayo maji wakaanza kuyachuja mpaka kutengeneza mikate sisi tunashindwaje kulima badala ya kuendelea kuagiza ngano nje ya nchi, kwanini kwa akili yake tusiwe na watu hata watatu wawekeze na tuwe na ngano ambayo hatuiagizi kutoka nje na hao vijana sasa waajiriwe kulima kwa hao watu au walime wapeleke malighafi?,” alihoji Kitwanga.
Aidha Kitwanga ameongeza kuwa, “achilia mbali hilo kuna sukari hivi sisi tunaagizaje sukari nje? una bodi ya sukari ni ya nini hawana maana kupanga bei ya sukari, hawafikirii kupanga mambo ya kilimo, ila wanawaza kuagiza nje Rais vunja hiyo bodi kila miaka inajadili bei badala ya kujadili kulima miwa kwa wingi kutengeneza sukari yetu, hivi tuna akili kweli sisi? tunaonekanaje.”