Kiwango cha maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kitaifa kimeshuka kutoka asilimia 7 mwaka 2003/04 hadi kufikia asilimia 4.7 mwaka 2016/17 huku maambukizi kwa wanaume ikiwa ni asilimia 3.4 na wanawake ni asilimia 6.3.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Zainab Chaula wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya mpango wa taifa wa kudhibiti Upungufu wa Kinga Mwilini (UKIMWI), ya mwaka 2018/19 kwa kamati ya kudumu ya Bunge ya masuala ya UKIMWI jijini Dodoma.
Amesema kiwango hicho cha maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kimeonekana kushuka kufuatia utafiti wa hali ya maambukizi nchini na kudai kuwa Wizara kupitia NACP inatekeleza mpango mkakati wa nne wa VVU na UKIMWI ambao unalenga kutekeleza malengo ya dunia ya 90 tatu (90 90 90).
“Mpango huu wa mkakati wa nne wa VVU na UKIMWI utatekeleza mpango wenye mwelekeo wa kupambana na ugonjwa wa Upungufu wa Kinga Mwilini yaani UKIMWI na unapaswa kufikiwa ifikapo mwaka 2020, “ ameongeza Dkt. Chaula.
Amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi Juni, 2019 Serikali kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi imetekeleza hatua mbalimbali kwa lengo la kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
Dkt. Chaula amesema hatua hizo ni pamoja na huduma za ushauri nasaha na upimaji, huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU na huduma za upimaji wa wingi wa VVU mwilini.
“Huduma zingine ni za tohara ya kitabibu kwa wanaume, huduma za kondomu, huduma za VVU na UKIMWI kwa makundi maalum na huduma za Habari, Elimu na mawasiliano ya kubadili tabia,” amefafanua Dkt. Chaula.