Imefahamika kuwa sababu za Mshambuliaji Adam Salamba kuachana na klabu ya JS Saoura, ni kushindwa kuonyesha makali yake tangu walipomsajili miezi minne iliyopita.
Mkataba wa Salamba na klabu hiyo umeripotiwa kuvunjwa rasmi Ijumaa (Februari 11) kufutia benchi la ufundi la timu hiyo linaloongozwa na Kais Yakoubi kutoridhishwa na kiwango chake licha ya awali kufanya vizuri kabla ya msimu kuanza.
Ripoti kutoka Algeria inasema kuwa:” Salamba amejikuta akicheza michezo mitatu tu ya ushindani akiwa na klabu hiyo ndani ya miezi yake minne huku akishindwa kutupia bao hata moja, alikuwa kama mzigo ndani ya klabu hiyo kiasi cha kuibuka kwa mvutano baina ya baadhi ya viongozi na benchi la ufundi kufuatia hasara ambayo wameingia kuvunja mkataba wake uliokuwa ukirajiwa kumalizika hadi mwishoni mwa msimu huu.
Klabla ya kuondoka nchini na kutimkia Algeria, Salamba alikuwa akiwatumikia Namungo FC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara, huku klabu nyingine alizowahi kuzichezea katika ligi hiyo ni Simba SC, Lipuli FC na Stand United.