Mwenyekiti wa Bodi ya Tumbaku, Victor Mwambalaswa amesema uzalishaji wa tumbaku nchini umeongezeka kutoka kilo milioni 60 hadi kilo milioni 108 na kwamba Kimkoa, uzalishaji huo umeongezeka kutoka kilo 500,000 hadi kilo milioni 9.2.
Mwambalaswa ameyasema hayo wakati Waziri Mkuu alipokuwa akizungumza na wadau wa zao la tumbaku wilayani Namtumbo kwenye ukumbi wa shule ya sekondari ya Nasuli, Ruvuma yaliyowajumuisha wakulima, wanunuzi, wenye viwanda, maafisa kilimo, wasambazaji mbolea na wenye mabenki.
Amesema, ongezeko hilo la uzalishaji linahitaji kuongezwa kwa miundombinu ya mabani, vichanja na maafisa ugani wa kuwasaidia wakulima, na kwamba imesaidia kuongeza pato la mkulima mmoja mmoja na hata Serikali kupitia ukusanyaji wa kodi ambazo humsaidia mwananchi kupata huduma za kijamii.
Kwa upande wake, Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kufungua mahusiano ya kibiashara na nchi za nje, hali ambayo imesaidia kupata wanunuzi wa zao hilo, huku baadhi ya wafanyabiashara wakiomba kuimarishwa kwa njia kuu za masoko yaliyo na uhakika.