Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema Serikali iko katika hatua za mwisho kuanza uzalishaji katika Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira- Kabulo ili Serikali iweze kunufaika na makaa hayo.
Dkt. Biteko amesema hayo Julai 2, 2022 wakati wa ziara yake ya kutembelea mgodi wa Kiwira- Kabulo kukagua shughuli za uchimbaji wa makaa ya mawe na kuzungumza na wananchi wanaowazunguka mgodi huo katika wilaya ya Ileje Mkoani Songwe.
Amesema, tayari Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) imesaini mkataba na Kampuni ya ABSA ya nchini Uswiss ambapo tani 60,000 za makaa ya mawe zitauzwa kwa wawekezaji hao.
Dkt. Biteko amesema kuwa, Serikali imeharakisha kuanza kwa mchakato wa kufufua kiwanda hicho cha makaa ya mawe kinachomilikiwa na STAMICO ili kuleta heshima kubwa kwa watanzania.
“Kuna kitu kizuri kinakuja ndio maana tumewekeza fedha katika mradi huu, nataka niwaambieni tuwe na subra na nimesikiliza changamoto za wananchi Serikali itazifanyia kazi ili zitatuliwe mapema,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema, Serikali inatambua madai ya watumishi hivyo kwa sasa inashughulikia suala hilo ili malipo hayo yaweze kulipwa.
Amesema, kuanza kwa uzalishaji katika mgodi huo kutafungua fursa za kiuchumi, ajira za moja kwa moja kwa Watanzania na kuongezeka kwa Pato la Taifa.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amesema lengo ni mgodi huo kuanza uzalishaji mkubwa ili kukidhi mahitaji ya masoko makubwa nje ya nchi kupitia Bandari ya Mtwara.
Aliongeza kuwa, ili kuboresha uzalishaji Shirika limeagiza mitambo kwa ajili ya uchimbaji na uchakataji wa Makaa ya mawe licha ya kuwepo kwa changamoto ya miundombinu mibovu.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ileje Mkoa wa Songwe, Anna Gidalya amesema kuwa, kusimama kwa mradi huo kumepunguza ajira kwa vijana na kupunguza mapato ya halmashauri.
”Tunashukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kufufua mradi huo ambao utanufaisha wananchi wa wilaya za Ileje, Kyela na Rungwe ambao ni majirani zetu,” alisema.