Wakati baadhi ya watuhumiwa mbalimbali wa kesi za uhujumu uchumi wakiwa tayari wamekiri na kulipa faini pamoja na fidia kama mahakama husika zilivyohukumu, kompyuta zinazodaiwa kuhifadhi kumbukumbu za kesi hiyo katika ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) zimeibwa.

Kamanda wa Kanda maalum ya kipolisi, Dar Es Salaam, Lazaro Mambosasa amekiri kwa njia ya simu kwamba tukio hilo ni la kweli na kwamba hadi sasa hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusika na tukio hilo

Akiongezea amesema kuwa jeshi la polisi linaendela na uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo.

Kwa mujibu wa gazeti la Nipashe inadaiwa kuwa mnamo Oktoba 15 mwaka huu ilibainika kuibwa kwa kompyuta hizo zenye baadhi ya kesi za wahujumu uchumi.

Tukio hilo limetokea ofisi hiyo ikiwa katika mchakato wa kujadiliana na kuingia makubaliano na watuhumiwa mbalimbali wa kesi za uhujumu uchumi na utakatishaji fedha.

Ambapo baadhi ya kesi zilizokwepo katika hatua ya makubaliano ni pamoja na vigogo wa IPTL, Harbinder Sethi na James Rugemarila, ambao wanadaiwa kutakatisha zaidi ya Sh.bilioni 309, watuhumiwa wengine ni mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera anayetuhumiwa kutakatisha jumla ya milioni 173, mwingine ni Yusuf Ally maarufu kama Mpemba wa Magufuli anayetuhumiwa kusafirisha nyara za Serikali zenye thamani zaidi ya Shilingi Milioni 200.

Aidha ofisi hiyo wiki mbili zilizopita imeingiza zaidi ya bilioni 40 ambapo bilioni 3.6 zimepokelewa na zilizobaki wahusika wameahidi kulipa kwa mujibu wa makubaliano yao.

 

 

 

BAKITA yatoa maana ya neno Kisulisuli
Kama bado unatafuta ajira, hizi hapa nafasi za kazi kutoka makampuni 10 Tanzania