Mwanamke mmoja jijini New York nchini Marekani amedai kubakwa na bosi wake katika ofisi yake ndani ya jengo la klabu ya usiku ya Kijapani inayojulikana kama Usagi.
Kwa mujibu wa taarifa za mashtaka yaliyowasilishwa Katika Mahakama ya Juu ya Manhattan, mwanaume huyo aliyetajwa kwa jina la Hazumu Suzuki ambaye ni meneja wa klabu hiyo alimueleza msichana huyo kuwa anamuomba abaki ofisini ili wajadili masuala ya kazi, lakini baada ya kubaki alimvamia na kumuangusha sakafuni kabla hajamvua nguo kwa nguvu na kumbaka.
Mwanamke huyo alidai kuwa alifanya jitihada za kupiga kelele na kujihami lakini hakufanikiwa kupata msaada wowote. Nguo zilizochanwa katika tukio hilo zilikabidhiwa kwa polisi ambao wameeleza kuwa wanaendelea na upelelezi.
Katika maelezo yake, mwanamke huyo alidai kuwa awali aliripoti kwa mmiliki wa klabu hiyo, Atsuko Kinoshita ambaye alikiri kuwa meneja huyo alikuwa na tabia ya kufanya fujo anapolewa na kwamba alikuwa akipata majeraha ambayo asubuhi alieleza kuwa hafahamu kilichomtokea.
Kwa mujibu wa New York Post, mmiliki wa klabu ya Usagi alieleza kuwa alimuongezea mkataba wa kazi Suzuki ili aweze kupata sifa za kuongeza muda wa Visa yake nchini Marekani.
Mmiliki wa klabu hiyo pia ni mmoja ya washtakiwa katika kesi hiyo akidaiwa kuendelea kumuajiri Suzuki licha ya kujua kuwa alikuwa na tabia ya kuwadhuru wanawake anapolewa.
Mwanamke aliyefungua mashtaka hayo anadai pia fidia ya dola milioni 10 ($10 million) kutokana na tukio hilo.