Mali za aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Hayati Robert Mugabe, zimewekwa wazi na kubainika kuwa aliacha kiasi cha dola milioni 10 na baadhi ya mali nyingine za thamani ambazo zipo Harare nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka gazeti la Serikali la Herald imeelezwa kuwa licha ya Mugabe kuwa na utajiri mkubwa, hakuacha wosia wowote au tamko kuhusu warithi wa mali hizo.
Kiongozi huyo ambaye alifariki septemba mwaka huu, alikuwa anatetwa na wananchi wake juu ya kiasi cha utajiri alichonacho huku wengi wakidhania kuwa yeye na familia yake wamejilimbikizia utajiri mkubwa ambao aliupata kwa miaka 37 aliyokaa madarakani.
Binti yake, Bona Chikowore mwezi oktoba aliiandikia barua Mahakama kuu ya Zimbabwe, akitaka kuandikisha mali za hayati baba yake.
Mali hizo zinajumisha fedha tasilimu dola milioni kumi ambazo zipo kwenye benki nchini humo, nyumba nne ambazo zipo harare, magari kumi, shamba moja, nyumba moja ya kijijini na bustani ya miti.
Gazeti hilo limeandika kuwa orodha iliyotolewa haijajumuisha mashamba kadhaa ambayo yanatajwa kuwa mali ya Mugabe au biashara ya maziwa ambayo ilikuwa ikifanywa na mkewe Grece pamoja na mali nyingine zilizo nje ya nchi.
Katika hatua nyungine, wakili wa hayati Mugabe aliiomba Mahakama kuzisajili mali za Rais huyo kwa madai kuwa yeye na familia ya Mugabe hawajapata waraka wowote ulioachwa.
Ikumbukwe kuwa, sheria za Zimbabwe zinaeleza kuwa mali za mtu anayefariki dunia bila kuacha wosia wowote hugawiwia mke na watoto wake.