Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limeingilia kati na kusimamisha maandamano na vurugu zilizotokea katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Konde zilizohusisha waumini wa kanisa hilo.
Ofisa Operesheni wa Jeshi la Polisi, Johanes Bitegeko akiwa na askari wengine waliingia maeneo ya kanisa hilo na kuwatawanya waumini waliokuwa wamekusanyika makundi mawili tofauti wanaomuunga mkono Askofu Mwakihaba na Dk Mwaikali.
Akizungumza eneo la tukio, Bitegeko amesema mgogoro huo umekuwa wa muda mrefu na kuwataka watu wote kutawanyika akisema bado unashughulikiwa.
“Sina mambo mengi, kazi yetu ni kushughulikia usalama, mmekusanyika bila sababu za msingi tunaomba muondoke muendelee na shughuli za uzalishaji,” alisema Ofisa huyo.
Mchungaji wa Jimbo Kuu la Mbeya Mashariki, Lugano Mwakasege aliyekuwa pamoja na waumini hao wakati wa vurugu hizo ameelezea sababu za kufunga kanisa la KKKT Ruanda Dayosisi ya Konde mkoani Mbeya kuwa ni kushtushwa na tangazo la aliyekuwa mchungaji wa kanisa hilo ndugu Mwambola pamoja na Askofu Mwaikale kutangaza kuwa wamehama kanisa.
“Kilichotufanya tuje hapa leo asubuhi ni kuwa aliyekuwa mkuu wa jimbo, mchungaji wa kanisa hili ambaye sasa ameshavuliwa akiwa na ndugu Mwaikale walisimama na kutangaza kuwa wao kwa sasa wamehamia kanisa la Kirutheri Afrika Mashariki. Sisi kanisa letu ni KKKT Dayosisi ya Konde,” alisema Mchungaji Mwakasege.
“Kwa hiyo leo ndio nimewahi hapa ofisini pamoja na kufunga ofisi hizi kwa sasa tuna ofisi moja ipo Tukuyu nido makao makuu yetu ya Jimbo na sasa hata ofisi ya Jimbo haipo tena hapa.” aliongeza.
Kanisa hilo ambalo alikuwa anatumia aliyekuwa Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Konde, Dk Edward Mwaikali kama makao makuu limefungwa leo Jumatatu Juni 13, 2022 na waumini wanaomuunga mkono Askofu Geofrey Mwakihaba.
Wiki moja baada ya kuvuliwa madaraka, aliyekuwa askofu wa Dayosisi ya Konde ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Edward Mwaikali na baadhi ya wachungaji na waumini wamejitenga na kanisa hilo.
Uamuzi huo ulitangazwa jana katika Kanisa Kuu la Ruanda jijini Mbeya na Dk Mwaikali aliyesema yeye, wachungaji na waumini wanaomuunga mkono sasa watakuwa wanaabudu katika Kanisa la Kiinjili Afrika Mashariki (KKAM).
KKAM lilianzishwa mwaka 1999 na kupata usajili mwaka 2005 na tayari limepanuka na kusambaa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Manyara, Singida, Tabora, Shinyanga, Dar es Salaam na lipo katika hatua za mwisho kuanzisha tawi mkoani Mwanza.