Mchezo wa pili hatua ya fainali ya ligi ya mabingwa Amerika ya kusini unaowakutanisha manguli wa soka duniani Boca Juniors na River Plate, umehamishiwa nchini Qatar, baada ya kushindwa kufanyika nchini Argentina kufuatia fujo zilizokwamisha pambano hilo mara mbili mfululizo.
Shirikisho la soka Amerika ya kusini (CONMEBOL), limetangaza maamuzi hayo baada ya kamati kuu kukutana jana, na kuona kuna umuhimu wa mchezo huo ambao utamtoa bingwa wa bara hilo upande wa klabu kuchezewa nchini Qatar kwenye uwanja wa kimataifa wa Khalifa (Khalifa International Stadium) uliopo mjini Doha.
Uwanja wa kimataifa wa Khalifa una sifa ya kuchukua mashabiki 40,000 walioketi, na utatumika kwenye fainali za kombe la dunia za mwaka 2022.
Dhamira kubwa ya kupeleka mchezo huo nchini Qatar ni kukwepa zogo nla mashabiki wa pande hizo mbili ambalo lilionekana kuwa kero, katika mji wa Buenos Aires majuma mawili yaliyopita.
Mchezo huo umepangwa kucheza Desemba 08, na klabu zote mbili zitalazimika kusafiri umbali wa maili 8,268 kutoka mjini Buenos Aires kwa ajili ya kumalizia kiporo cha mchezo huo wa fainali.
Mshindi wa mchezo huo atalazimika kusalia mashariki ya kati kwa ajili ya kuendelea na michuano ya klabu bingwa duniani (FIFA Club World Cup) ambayo itaanza mjini Abu Dhabi, siku nne baada ya kipyenga cha mwisho kupulizwa Desemba 08.
Khalifa International Stadium
Hata hivyo taarifa za tetesi zinadai kuwa uongozi wa klabu ya Boca Junior huenda ukagoma kushiriki kwenye mchezo huo, kwa madai walistahili kupewa ubingwa, kutokana na zogo lililojitokeza Buenos Aires, mwishoni mwa juma lililopita kabla ya mchezo wa pili.
Uongozi wa klabu hiyo unadai lililojitokeza kabla ya mchezo huo lilisababishwa na mashabiki wa River Plate.
Katika mchezo wa kwanza wababe hao wa mjini Buenos Aires walitoka sare ya kufungana mabao mawili kwa mawili.
Uwanja wa kimataifa wa Khalifa umekua uwanja wa kwanza kukamilika kwa wakati, kwa ajili ya fainali za kombe la dunia 2022, na umetumia kiasi Paundi milion 70 kwa ajili yakufanyiwa maboresho, kabla ya kufunguliwa rasmi mwaka 2017.
Shirikisho la mchezo wa riadha duniani IAAF limetangaza kutarajia kuutumia uwanja huo kwa ajili ya michuano ya dunia ya riadha mwaka 2019 itakayofanyika kuanzia mwishoni mwa mwezi Septemba hadi mwanzoni mwa mwezi Oktoba.