Baada ya chenga nyingi za Klabu ya Simba kuhusu kiasi cha pesa ilichopokea kumuuza aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Emmanuel Okwi, sasa ‘wazungu’ wa Denmark wameweka mambo hadharani.

Klabu ya ya SønderjyskE ya nchini Denmark imeiambia dunia kuwa imeilipa Klabu ya Simba kiasi cha Shilingi za Tanzania takribani milioni 220 ($ 110,000) kama malipo ya kumhamishia Emmanuel Okwi Klabuni hapo. Uongozi wa klabu hiyo umemsainisha Okwi mkataba wa kipindi cha miaka mitano.

Awali, Klabu ya Simba kupitia Kaimu Katibu Mkuu wake, Collins Frisch ilikataa kutaja kiasi walichopokea kumuachia Okwi, suala walilolibeba kama siri kubwa.

Baadae, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe naye aliamua kumwaga mchele kwenye kuku wengi baada ya kuona mchele wenyewe ushaamwagwa na upande wa pili.

“Kweli hicho ndicho kiasi tulichokubaliana kulipwa, katikati ya mwezi huu nafikiri tarehe 17 watatulipa,” Poppe alithibitisha.

Tayari Okwi ameichezea timu hiyo ya Denmark kwa dakika 76 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Schleswigers.

Hasheem Thabeet Ashauriwa Kusaka Timu Uturuki
Babu Hans Apangua Upya Kikosi Cha Yanga