Baadhi ya klabu za soka nchini Tanzania zimetuma salamu za rambirambi kwa Watanzania na familia ya aliyekuwa Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ambaye amefariki dunia usiku wa kuamkia leo, Julai 24, 2020 jijini Dar es Salaam.
Klabu kongwe za Simba na Young Africans ni miongoni mwa klabu zilizotuma salamu hizo kupitia kurasa za mitandao ya kijamii kufuatia kifo hicho na pole kwa mjane wa Rais huyo mstaafu, Mama Anna Mkapa, familia, ndugu na Watanzania wote.
Ukurasa wa Instagram wa Young Africans imetoa taarifa za masikitiko kufuatia msiba huo wa taifa.
“Young Africans Sports Club tumepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin William Mkapa,” ulisomeka ujumbe wa Klabu ya Yanga.
Kwa upande wa klabu ya Simba nayo imetoa pole kwa watu wote walioguswa na msiba huo.
“Simba SC tunatoa pole kwa familia, ndugu, marafiki na Watanzania wote kwa msiba huu mkubwa kwa Taifa letu. Tunamuombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi. Amin.”
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ya Tanzania ikimnukuu Rais John Magufuli imeeleza kuwa Rais mstaafu Mkapa alikuwa amelazwa jijini hapa. Kufuatia kifo cha Rais huyo mstaafu, Rais Magufuli ametangaza siku saba za maombolezo ambapo bendera zote zitapepea nusu mlingoti.
“Kwa masikitiko makubwa tumepata msiba mkubwa, Mzee wetu Benjamin William Mkapa, Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu amefariki dunia katika hospitali jijini Dar es Salaam ambako alikuwa amelazwa, niwaombe Watanzania tulipokee hili, tumepata msiba mkubwa tuendelee kumuombea mzee wetu ambaye ametangulia mbele za haki,” amesema Rais Magufuli
Pia Rais Magufuli amewataka Watanzania kuwa wastahimilivu baada ya kupokea taarifa za msiba huo mzito.
Rais mstaafu Mkapa alizaliwa Novemba 1938 wilayani Masasi mkoani Mtwara, ambapo aliiongoza nchi kwa awamu mbili kuanzia mwaka 1995-2005.