Mkoa wa Dodoma unaendeleza jitihada ya kuondosha migogoro ya Ardhi, kwa kuanzisha Kliniki ya kusikiliza kero na malalamiko ya Wananchi kuhusu Ardhi pamoja na kuwapatia hati zao wale wote wanaokidhi vigezo vinavyohitajika
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ameyasema hayo hii leo Oktoba 19,2023 wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kata ya Ihumwa Jijini Dodoma, inayolenga kusikiliza na kuzitatua kero mbalimbali za Wananchi katika Kata hiyo.
Amesema, Kliniki hiyo itakuwa ni endelevu na kwamba Wakazi wa Kata hiyo wanatakiwa kutumia fursa ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali, ikiwemo Reli ya kisasa – SGR, pamoja na Barabara ya Mzunguko kama fursa ya kujiongezea na vipato.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri amesema hali ya usalama katika maeneo ya kata hiyo kwa sasa ni shwari na kuwataka Wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kujilinda ili kuendeleza usalama katika maeneo yao.
Awali, Diwani wa Kata ya Ihumwa, Edward Magawa alisema kwa sasa wameshaanza Ujenzi wa kituo cha Polisi ili kuhakikisha hali ya ulinzi na usalama inaendelea kuimarika na kuepuka vitendo vya kiuhalifu vinavyojitokeza mara kwa mara katika maeneo yao.