Eva Godwin – Dodoma.
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na jiji la Dodoma imetoa Hati Miliki za ardhi 3,156 na kuwahudumia wananchi 7363 waliofika kwenye Kliniki ya Ardhi na kuongeza mapato ya Serikali zaidi ya Shilingi 600 Milioni.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda wakati akitoa tathmini ya Kliniki ya ardhi iliyoendeshwa jijini Dodoma kuanzia Novemba 4, 2023 ya kutatua migogoro ya ardhi katika ili kutekeleza maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha migogoro ya ardhi inapatiwa ufumbuzi.
Amesema, katika zoezi hilo jumla ya maombi mapya 2,433 ya umilikishaji wa ardhi yamepokelewa huku namba za malipo (control No) 8,539 zimetolewa na kuingizia Serikali kiasi cha Shilingi 691,250,626.90 na kudai kuwa huo ni mpango wa Wizara unaoendeshwa nchi nzima kweye ofisi za ardhi za Mikoa na Halmashauri.
Kwa upande wao baadhi ya wanufaika wa Kliniki hiyo, akiwemo Mwenyekiti wa Mtaa wa Mahoma Makulu Kata ya Chawa, Jerome Petro na Asia Jabu Maalim kutoka Barabara ya 7 kata ya Madukani wamesema, Kliniki hiyo imewasaidia wananchi wa Dodoma kwa kupata huduma za kupata hati za viwanja vyao tofauti na hali ilivyokuwa kabla ya kliniki hiyo.