Mshambuliaji kutoka nchini Misri Mohamed Salah, alitarajiwa kuanza mazoezi leo Jumatatu (Novemba 23), baada ya kufanyiwa vipimo na kubainika hana tena maambukizi ya virusi vya Corona.

Salah aligundulika kuwa na maambukizi ya virusi vya Corona, juma lililopita aliporejea Misri kwa ajili ya kuitumikia timu ya taifa kwenye michezo ya kuwania kufuzu fainali za Afrika (AFCON 2022).

Meneja wa Liverpool, Jurgen Klopp amesema anatarajia kumuona mshambuliaji huyo mazoezini, na ana matumaini ya kumtumia kwenye michezo ya Ligi na ile ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Salah alikosa mchezo wa Ligi Kuu ya England dhidi ya Leicester City jana Jumapili, na alitarajiwa angeendelea kujitenga na wenzake (Karantini) kwa siku 10 zaidi.

Klopp amesema amehakikishiwa kuwa Salah hana tena maambukizi ya virusi vya Corona, lakini akasisitiza kuwa kabla ya kuanza mazoezi atafanyiwa tena vipimo.

“Nimesikia kuwa leo ameonekana hana maambukizi. Nadhani kuanzia sasa yupo kawaida baada ya vipimo vyote. Kesho tutakuwa na vipimo vya UEFA.”

“Anaweza kuanza mazoezi na sisi kesho. Kutakuwa na vipimo viwili zaidi katika siku mbili zijazo.”

Mpaka sasa, kwa mujibu wa taaratibu za Shirikisho la soka Barani Ulaya (UEFA), mshambuliaji huyo ambaye tayari ameshafunga magoli 10 kwenye mechi 13 anaweza kushiriki mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Atalanta keshokutwa Jumatano.

Azam FC yaitangazia njaa Young Africans
Iran yaapa ‘kuichapa’ Israel ikifanya haya mwaka huu