Mshambuliaji anaeshikilia rekodi ya kufunga mabao mengi katika fainali za kombe la dunia Miroslav Klose, ametangaza kustaafu soka baada ya kuutumikia mchezo huo kwa muda wa miaka 18.

Klose amefunga mabao 16 katika fainali za kombe la dunia akiwa na timu ya taifa lake la Ujerumani, jambo ambalo limemfanya aendelee kutajwa kuwa mbora zaidi kwenye michuano hiyo, baada ya kumpiku aliyekua mshambuliaji wa timu ya taifa ya Brazil Ronaldo.

Klose pia anashikilia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote kwa upande wa timu ya taifa lake la Ujerumani, baada ya kuzifumania nyavu mara 71, katika michezo 137.

Hata hivyo aliyekua kiungo na nahodha wa timu ya taifa ya Ujerumani Lothar Matthaus ameendelea kushika rekodi ya kucheza michezo mingi zaidi, kwani mpaka anastaafu soka la kimataifa mwaka 2000 alikua ameitumikia DFB Eleven michezo 150.

“Ninashehekea mafanikio yangu makubwa nikiwa na timu yangu ya taifa,” Alisema Klose. “Kwa muda huo ilikua ni nafasi nzuri kwangu kutimiza wajibu wa kucheza kwa uweledi, daima sitosahau maishani mwangu.”

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 38, aliyeachwa na klabu ya SS Lazio mwishoni mwa msimu uliopita, anatarajiwa kujumuika na wachezaji wa timu ya taifa ya Ujerumani katika maandalizi ya mchezo ujao wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia, kwa ajili ya kupewa heshima za mwisho na kuwaaga mashabiki.

“Sina budi kumshukuru kocha Jogi Low pamoja na Hansi Flick (Mkurugenzi wa Michezo) kwa nafasi waliyonipa,” ilieleza taarifa ya Klose ambayo ilitolewa na chama cha soka nchini Ujerumani.

Mafanikio ya Klose kabla hajatangaza kustaafu soka.

Kwa upande wa klabu.

  • Ubingwa wa ligi ya Ujerumani mara mbili (Bundesliga) (Bayern, 2007-08 na 2009-10)
  • Kombe la Ujerumani mara mbili (Bayern, 2007-08 na 2009-10)
  • Kombe la Italia – Coppa Italia (SS Lazio, 2012-13)
  • Medali ya mshindi wa pili ligi ya mabingwa (Bayern, 2009-10)

Upande wa timu ya taifa:

  • Ubingwa wa kombe la dunia (2014)
  • Medali ya mshindi wa pili kombe la dunia (2002)
  • Medali ya mshindi wa pili kombe la Ulaya (2008)
  • Tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Ujerumani (2006)
  • Kiatu cha dhahabu ufungaji bora – kombe la dunia (2006)
  • Kiatu cha Fedha ufungaji bora – Kombe la dunia(2002)

Bakora Ya FA Yamchapa David Moyes
Live: Tazama Bunge la 11 leo Novemba 2, 2016