Timu ya KMC FC kesho Alhamis (Desemba 15) itafungua rasmi mzunguuko wa Pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuikaribisha Coastal Union Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.
Mchezo huo uliopangwa kuanza saa kumi jioni, utashuhudia wenyeji KMC FC wakipambana kwa kuhitaji alama tatu muhimu, huku wapinzani wao waliofunga safari kutoka Tanga, nao watahitaji ushindi ili kujiweka katika mazingira mazuri katika kipindi hiki cha lala salama.
Kocha Mkuu wa KMC FC Thierry Hitimana amesema tayari kikosi chake kimeshakamilisha maandalizi ya mchezo huo na wachezaji wote wapo tayari, kuikabili Coastal Union na kuibuka na ushindi.
Hitimana amesema kuwa kama kikosi chake kimejipanga vizuri kutokana na kwamba michezo ya mwisho haikuwa na matokeo mazuri na hivyo changamoto kubwa ilitokana na wachezaji wengi kuwa na majeraha lakini kwasasa wanne wamerejea jambo ambalo limeleta matumaini makubwa.
“Tunafahamu kuwa mzunguko wa pili utakuwa na ushindani zaidi kutokana na kwamba kila Timu inahitaji kufanya vizuri na hivyo tunakwenda kupambana ili tupate matokeo mazuri kwakuwa michezo yote ipo ndani ya uwezo wetu.
Hata hivyo Hitimana amesema kuwa KMC FC itawakosa wachezaji wawili ambao ni Hance Masoud pamoja na Emmanuel Mvuyekure kutokana na chamgamoto za majeraha na kwamba wengine wapo kwenye ari na morali nzuri tayari kutumika kwa ajili kupata alama tatu.
“Coastal Union ni Timu nzuri hata ukiangalia katika mchezo wao wa mwisho walipata ushindi wakiwa ugenini, lakini hatuliangalii hilo kama changamoto badala yake tunajiandaa kwa ajili kuhakikisha kuwa tunatumia vizuri uwanja wetu wa nyumbani hapo kesho.” amesema Hitimana
KMC FC ipo nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 16, huku Coastal Union Ikishika nafasi ya 12 kwa kufikisha alama 15.