Klabu ya KMC FC imejinasibu kuwa tayari kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ambao utashuhudia wakicheza dhidi ya Azam FC kesho Ijumaa (Oktoba 21) katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam, kuanzia majira ya saa kumi jioni.
KMC FC inayonolewa na Kocha Thierry Hitimana imesisitiza kukamilisha maandalizi ya kuelekea mchezo huo, huku Idara ya Habari na Mawasilino ya klabu hiyo ikithibitisha kuwa Wachezaji wote wapo tayari kwa mtanange huo.
Afisa Habari wa KMC FC Christina Mwagala amesema, katika mchezo huo ambao watakua nyumbani, Kikosi chao kimejiandaa kikamilifu kuziwania alama tatu muhimu, lakini amekiri kuwa wanatarajiwa ushindani kutoka kwa wapinzani wao kutoka Chamazi jijini Dar es salaam.
“Tunakwenda kwenye mchezo wenye ushindani mkubwa , ambao tunahitaji ushindi, Azam ni Timu nzuri , wanawachezaji wazuri hivyo tunawaheshimu lakini KMC ni bora zaidi na kwamba kila mchezaji amejiandaa kutumika vizuri ili kupata alama tatu.”
“Tunajivunia kuwa na wachezaji wenye ubora na ambao siku zote wamekuwa wakijitoa kwa ajili ya Manispaa ya Kinondoni, kila mmoja anafahamu umuhimu wa mchezo huo , hivyo wana Kinondoni wote, mashabiki zetu kutoka maeneo mbalimbali mjitokeze kwa wingi kuwasapoti wachezaji wetu.”
“Kwa upande wa Afya za wachezaji wote wapo nzuri, morali na nguvu ya kutumika kwa ufanisi mkubwa, hivyo mashabiki wasiwe na hofu Benchi la Ufundi limefanya kazi kubwa ya kuwaanda wachezaji kwa mafanikio makubwa yakuleta matokeo chanya.” amesema Christina
KMC FC inakwenda kwenye mchezo huo ikiwa katika nafasi ya sita kwenye Msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kucheza michezo saba, ikishinda michezo miwili na kuambulia sare mara minne huku ikipoteza mchezo mmoja, hali ambayo imeifanya kukusanya alama 10 hadi sasa.