Kikosi cha KMC FC leo Alhamis (Desemba 10) kinaelekea mjini Morogoro, tayari kwa mchezo wa mzunguuko wa 15 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar.
KMC FC itakua na kazi ya kusaka alama tatu muhimu za mchezo huo utakaochezwa kesho Ijumaa (Desemba 11), Uwanja wa Jamuhuri ikiwa ni hitaji la kuendeleza ubabe wa kufanya hivyo, kama ilivyokua mwishoni mwa juma lililopita walipoifunga Dododma Jiji FC, Uwanja wa Uhuru Dar es salaam.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino KMC FC Christina Mwagala amesema kikosi chao kimefanya maandalizi ya kutosha chini ya makocha wazawa John Simkoko akisaidiana na Habibu Kondo.
“Tunasafiri leo Ijumaa, tumejiandaa vizuri na tunaimani tutapambana kwenye mchezo wetu dhidi ya Mtibwa Sugar, na kupata matokeo chanya.”
“Tunawaheshimu Mtibwa Sugar, tunajua ni timu nzuri, lakini kikosi chetu hakina budi kupambana hiyo kesho na kupata matokeo yatakayoendelea kutupa furaha.”
“Hakuna mchezo ambao ni rahisi kwenye Ligi Kuu, lakini kwa maandalizi yaliofanywa na makocha wetu, nina imani wachezaji watapambana vizuri ndani ya dakika 90.” Amesema Christina Mwagala.
Kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, klabu ya KMC ipo nafasi ya tano ikiwa na alama 21, huku wapinzani wao Mtibwa Sugar wakishika nafasi ya 14 na alama 16.