Kikosi cha Wachezaji 22 wa KMC FC kimeondoka Jijini Dar es Salaam mapema leo asubuhi kuelekea Ruangwa Mkoani Lindi kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo utakaochezwa Jumapili ya (Mei 9, 2021) katika Uwanja wa Majaliwa Mkoani humo.

Kikosi hicho cha wana Kino Boys , kinakwenda kukutana na Namungo kwa mara ya pili katika msimu huu wa 2020/2021 huku KMC FC ikiwa ugenini ambapo awali katika mchezo ambao walikutana katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam ikiwa mwenyeji kikosi hicho kilipata ushindi wa magoli 3-0.

KMC FC chini ya Kocha Mkuu, John Simkoko pamoja na msaidizi wake Habibu Kondo wameendelea kukisuka kikosi hicho sambamba na kurekebisha makosa mbalimbali ambayo yalijitokeza katika mchezo wa michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam na hivyo kupelekea kutolewa katika michuano hiyo dhidi ya Dodoma Jiji ikiwa ni katika hatua ya kuweka mikakati kwa Timu ili iweze kufanya vizuri katika mchezo huo.

Hata hivyo katika michezo ya Ligi Kuu ambayo KMC FC imewahi kukutana dhidi ya Namungo, ikiwa ugenini, KMC FC ilipoteza mchezo mmoja kwa kufungwa magoli 2-1, huku Namungo wakipoteza michezo miwili wakiwa katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Imetolewa na Christina Mwagala, Afisa Habari na Mawasiliano wa Timu ya KMC FC.

Prof. Shemdoe atengua kitendawili cha uhamisho
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Mei 7, 2021