Kikosi cha KMC FC leo Ijumaa (Septemba 23) kimeanza maandalizi kuelekea mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara dhidi ya Namungo utakaopigwa Oktoba Mosi, katika uwanja wa Majaliwa Ruangwa Mkoani Lindi.
Kikosi hicho cha Manispaa ya Kinondoni chini ya kocha Mkuu Thierry Hitimana imeanza kujifua ikiwa ni baada ya kurejea kambini jana Alhamis (Septemba 22) majira ya jioni, baada ya kumaliza mapumziko ya siku mbili tangu ilipocheza mchezo dhidi ya Timu ya Ihefu Septemba 20, katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam ambapo KMC FC iliibuka na ushindi wa 2-1.
KMC FC kwa sasa inajiandaa na mchezo huo dhidi ya Namungo badala ya Mtibwa Sugar ambapo awali ulipangwa kuchezwa Septemba 27 kwa mujibu wa ratiba ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), kutokana na kubadilika kwa ratiba ambapo Septemba 21 ilitoa taarifa ya mabadiliko ya mchezo huo huku sababu ikielezwa kuwa baadhi ya timu zinazohusika kwenye michezo hiyo wachezaji wao wapo kwenye majukumu ya Timu ya Taifa.
“Tulipokea taarifa ya mabadiliko ya mchezo wetu dhidi ya Mtibwa Sugar ambao awali ilikuwa tucheze siku ya Jumanne ya Septemba 27 kwenye uwanja wetu wa Uhuru, kwa hiyo hivi sasa tunajiandaa kwa mchezo mwingine ambao tutakuwa ugenini dhidi ya Namungo Oktoba moja kule Ruangwa, hivyo tunajipanga vizuri kutafuta alama tatu muhimu ugenini.”
“Wachezaji wote wamesharejea kambini baada ya kumaliza mapumziko ya siku mbili ambayo tulitoa siku tuliyocheza mechi na Ihefu, na wote wamerejea salama wakiwa na nguvu, Afya njema, hari na morali kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunafanya maandalizi bora ambayo yatatupa matokeo chana kwenye mchezo huo licha ya kwamba tunafahamu fika hautakuwa mwepesi.” amesema Afisa Habari na Mawasiliano KMC FC Christina Mwagala
Hadi sasa KMC FC imecheza michezo minne ambapo kati ya hiyo tatu ikiwa ugenini huku mmoja ikiwa kwenye uwanja wa nyumbani, kati ya hiyo imeshinda mchezo mmoja dhidi ya Ihefu na kusare michezo miwili ambayo ni dhidi ya Simba pamoja na Polisi Tanzania huku ikipoteza dhidi ya Coastal Union.
Katika msimamo wa Ligi Kuu, KMC ipo kwenye nafasi ya nane ikiwa na jumla ya alama tano, magoli ya kufunga sita na magoli ya kufungwa sita, huku ikiendelea kujiimarisha zaidi kwenye michezo inayokuja ili kuhakikisha kuwa inapata matokeo mzuri.