Baada ya kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania jana Jumanne (Juni 14), Kikosi cha KMC FC kimerejea Kambini kuanza maandalizi ya mchezo ujao dhidi ya Wekundu wa Msimbazi Simba.

KMC FC itakua mgeni wa Simba SC Jumapili (Juni 19) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku ikikumbuka kichapo cha mabao 4-1 katika mchezo wa mzunguuko wa kwanza, uliopigwa Uwanja wa Alli Hassan Mwinyi Mkoani Tabora.

Afisa Habari na Mawasiliano KMC FC Christina Mwagala amesema maandalizi ya mchezo dhidi ya Simba SC yameanza rasmi leo Jumatano (Juni 15) chini ya Kocha Mkuu Thierry Hitimana, huku wakitambua wanakwenda kwenye mchezo mgumu, ambao kila mmoja anataka matokeo, lakini amewahakikishia mashabiki wa kuwa wanaenda kupambana uwanjani kuzisaka alama tatu muhimu.

“Jana hatujatimiza malengo ambayo tulihitaji kwa maana ya kupata alama tatu, lakini hiyo haitutoi kwenye mapambano , bado tunaendelea kujipanga zaidi kwa michezo inayokuja, tunafahamu kuwa mechi zilizobakia zote ni ngumu lakini tutahakikisha tunashinda.”

Upande wa Afya za wachezaji, Christina amesema kikosi chao hakina majeruhi, hivyo mashabiki na watanzania wote waendelee kuwasapoti kwa kuwa Ligi haijaisha na kwamba watahakikisha timu inamaliza Ligi kwenye nafasi nzuri.

Hadi sasa KMC imecheza michezo 26 na kukusanya jumla ya alama 32 zinzoiweka nafasi ya tisa kutoka nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Klabu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni imebakisha michezo ya Ligi Kuu msimu huu 2021/22 dhdi ya Simba SC, Mbeya Kwanza FC, Biashara United Mara pamoja na Dodoma Jiji FC.

Mkuu wa mkoa feki mikononi mwa Polisi
Wito wa utayari kushiriki zoezi la sensa