Baada ya kumalizana na Dodoma Jiji FC mwishoni mwa juma lililopita na kuambulia alama tatu muhimu, kikosi cha KMC FC kimeanza mipango na mikakati ya kuhakikisha wanaizima Mtibwa Sugar kwenye mchezo ujao wa Ligi Kuu utakaochezwa Desemba 11.
Mchezo huo wa mzunguuko wa 15 utachezwa Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro, huku KMC FC wakionyesha kuwa na hamu kubwa ya kuhakikisha wanapata ushindi ugenini.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino KMC FC Christina Mwagala amesema, tayari kikosi kimeanza maandalizi jijini Dar es salaam, chini ya kocha mzawa Habib Kondo akisaidiana na John Simkoko.
Amesema dhumuni kubwa ni kuendeleza wimbi la ushindi kwenye michezo ya Ligi Kuu, baada ya kufanya hivyo dhidi ya Dododma Jiji FC, siku ya Ijumaa, Desemba 04.
“Kwa sasa kikosi kimeanza maandalizi kwa ajili ya mchezo wetu dhidi ya Mtibwa Sugar na tuna amini kwamba tutapata matokeo chanya ndani ya uwanja ugenini.”
“Tunaamini kwamba mchezo utakuwa mgumu ila tupo tayari hasa ukizingatia kwamba kwa sasa wachezaji wamekuwa na shauku ya kupata ushindi ndani ya uwanja. Mashabiki waendelee kutupa sapoti imani yetu ni kwamba tutafanya vizuri na kila kitu kinawezekana.” Amesema Christina Mwagala.
Wakati KMC FC wakijiandaa kupata ushindi ugenini, wenyeji wao Mtibwa Sugar nao wameanza kujiwinda na mchezo huo, huku wakiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Mwadui FC, walioupata Jumapili,Uwanja wa Jamuhuri-Morogoro.