Baada ya kuambulia kisago cha mabao 2-0 dhidi ya Mabingwa watetezi Simba SC juzi (Jumatano 07), Kikosi cha KMC FC leo Ijumaa (Julai 09) kimerejea mazoezi kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu soka Tanzania bara dhidi ya JKT Tanzania utakaochezwa Jumanne (Julai 14) katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.

Kikosi hicho kinachonolewa na makocha , Kocha Mkuu John Simkoko pamoja na Habibu Kondo kinaendelea kujifua ikiwa ni baada ya kutoka kupoteza mchezo muhimu dhidi ya Simba uliopigwa katika Dimba la Benjamini Mkapata Julai 7 mwaka huu.

KMC FC ambayo hivi sasa imebakiza michezo miwili kabla ya kumalizika kwa msimu wa 2020/2021 imejipanga kuhakikisha kwamba licha ya kuwepo kwa ushindani mkubwa kuelekea kwenye mchezo huo, lakini inajipanga kupata matokeo mazuri kwa maana yakuondoka na alama tatu.

Afisa Habari na Mahusiano wa KMC FC ambayo ipo katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu soka Tanzania bara kwa kucheza michezo 32, Christina Mwagala amesema timu yao inajiandaa kufanya vizuri katika michezo miwili iliyosalia ambayo ni dhidi ya JKT Tanzania utakaochezwa Julai 14 pamoja na Ihefu mchezo ambao utapigwa Julai 18 katika Uwanja wa Uhuru hapa Jijini Dar es Salaam.

“Tumetoka kupoteza mchezo muhimu dhidi ya Simba, lakini hii haitutoi mchezoni kuelekea katika mchezo wetu mwingine muhimu, tunakutana na JKT Tanzania Julai 14, lakini tunajua mchezo huo utakuwa mgumu na sio huo tu hata ule dhidi ya Ihefu lakini tutahakikisha tunavuna alama zote sita.”

“Kwa sasa wachezaji wetu wote wapo vizuri pamoja na kwamba matokeo dhidi ya Simba yaliwaumiza lakini tunajipanga tena upya, na kikubwa chakuzingatia ni kwamba KMC FC ni Timu ambayo inamalengo makubwa hivyo tunapambana kwenye michezo hii iliyobaki tufanye vizuri ili msimu ujao tuanze na mikakati mipya”.

Hata hivyo Christina Mwagala ameongeza kuwa, wachezaji wote wako vizuri isipokuwa mchezaji Andrew Vicent Chikupe ambaye alipata kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Simba SC ambapo kama Timu itakosa huduma yake katika michezo miwili iliyobakia.

Tanzania kushirikiana na UNEP utunzaji mazingira
TPLB yatoa pole Polisi Tanzania FC