Kikosi cha timu ya KMC FC kimejinasibu kuwa tayari kwa mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa mchujo “Play Off’ dhidi ya Mbeya City itakayokuwa nyumbani katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya kesho Jumanne (Juni 13).
Kikosi cha KMC FC kimewasili jijini Mbeya kikotokea Sumbawanga Sumbawanga kilipokuwa na mchezo wa mwisho wa ligi kuu dhidi ya Mbeya City, ambao walikubali kichapo cha 1-0.
Afisa habari wa klabu hiyo, Christina Mwagala amesema maandalizi kuelekea mchezo huo yamekamilika na wachezaji wote wapo katika hali nzuri kuelekea kwenye mchezo huo muhimu.
“Tunafahamu mchezo utakuwa mgumu, lakini wachezaji wetu wameapa kukikishia kubaki ligi kuu msimu ujao, mchezo huu ni muhimu na wachezaji wetu wanatambua, kila mmoja akili ameelekeza kwenye mchezo huu kwa sababu hatutaki kushuka daraja,” amesema Christina
Aidha Christina amewaomba mashabiki wa timu hiyo kuendelea kushirikiana nao katika kipindi hiki kibaya lakini ana imani wao kama KMC FC watafanikiwa kubaki Ligi Kuu msimu ujao.
KMC FC imemaliza Ligi Kuu ikiwa katika nafasi ya 13 baada ya kujikusanyia alama 32 ikiwa ni alama moja zaidi ya Mbeya City iliyomaliza katika nafasi ya 14.
Timu itakayofungwa kwenye matokeo ya jumla baada ya michezo miwili itacheza na Mashujaa FC ya ligi daraja la kwanza kuwania kucheza ligi kuu msimu ujao.