Timu ya Manispaa ya Kinondoni ‘KMC FC’ inatarajia kurejea dimbani Juni 14, kukipiga na maafande wa Jeshi la Magereza Tanzania Prisons, katika mchezo wa Mzunguuko wa 27 wa Ligi kuu Tanzania Bara msimu huu 2021/22.

KMC FC yenye maskani yake jijini Dar es salaam, inajiandaa kuelekea kwenye mchezo huo ikiwa nafasi ya 10 katika msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 31, huku wapinzani wao Tanzania Prisons ikiwa nafasi ya 14 kwa kumiliki alama 25.

Afisa Habari wa KMC FC Christina Mwagala amesema maandalizi ya kikosi chao yanaendelea vizuri kwenye mchezo huo sambamba na michezo mingine minne ya mwisho ya msimu huu.

Amesema kikosi chao kimekua na maandalizi kabambe chini ya Kocha Thiery Hitimana, ili kufanikisha lengo la kuzikusanya alama zote 15, wakianza na Tanzania Prisons ambayo msimu huu imeonyesha udhaifu mkubwa wa kushindwa kupambana kama ilivyokua misimu iliyopita.

“Tumebakisha siku tano hadi siku ya mchezo wetu wa Tanzania Prisons, Kocha Hitimana na wasaidizi wake wameweka mkakati maalum wa kuhakikisha mambo yanatunyookea katika michezo yetu mitano iliyobaki, tukianza na huu wa Juni 14,”

“Mchezo huu dhidi ya Tanzania Prisons, tunafahamu haitakua rahisi kwa sabaabu wapinzani wetu wamejizatiti kuhakikisha wanashinda kama ilivyo kwetu sisi, lakini kwa kuzingatia hilo ndio maana KMC FC kupitia benchi letu la ufundi tumeweka maandalizi kabambe ya kikosi ili kufikia lengo la kuzipata alama tatu muhimu, tofauti na wenzetu,”

“Tumebakiwa na michezo mitano mkononi, na dhamira yetu ni kuzipata alama 15 za michezo hii ili kujisogeza katika nafasi nne za juu katika msimamo, hivyo hatutaki maskhara katika hili, tunaimani kubwa na Benchi letu la Ufundi litafikia lengo tulilojiwekea.” Amesema Mwagala

Susan Buffet Foundation kuipatia Tanzania Dola Milioni 15
Kagera Sugar yasaka alama 12 Ligi Kuu