Licha ya kupoteza mchezo wa awali wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika tena wakiwa nyumbani, wawakilishi wa Zanzibar kwenye michuano hiyo, KMKM wamesema wana matumaini makubwa ya kwenda kupindua matokeo ugenini na kutinga Raundi ya Kwanza.
Katika mchezo wa awali uliopigwa Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, ambao KMKM inautumia kama uwanja wake wa nyumbani kutokana na ule wa Amaan visiwani Zanzibar kuwa katika matengenezo, ilikubali kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya St George ya Ethiopia.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Ame Msimu, amesema tayari wamefanyia kazi mapungufu yote waliyoyaona katika timu yao kwenye mchezo wao uliopita, hivyo ana matumaini ya kufanya vizuri ugenini.
Amesema mapungufu makubwa waliyoyaona katika mchezo huo ni wachezaji kutozitumia vizuri nafasi walizotengeneza pamoja na kukosa umakini hasa wanapokuwa katika lango la mpinzani wao.
Amesema tayari mapungufu hayo yamefanyiwa kazi ikiwamo kuwapa somo la saikolojia wachezaji kutokuwa na hofu ya mchezo hasa wakiwa ugenini ili kutimiza lengo lao.
Hata hivyo, amesema timu hiyo itaendelea na kambi yake Tanzania Bara hadi watakapoelekea Ethiopia katika mchezo wa marudiano.
KMKM itashuka dimbani ugenini nchini Ethiopia Jumamosi (Agosti 26), ikihitaji kupata ushindi kuanzia mabao 2-0 ili kuweza kutinga Raundi ya Kwanza ya michuano hiyo inayoongoza kwa utajiri Barani Afrika kwa ngazi ya klabu.