Chama cha soka nchini Uholanzi KNVB huenda kikamtangaza meneja wa klabu ya Man Utd, Louis van Gaal kuwa mkurugenzi wa ufundi, endapo atasitishiwa mkataba wake na uongozi wa Man Utd mwishoni mwa msimu huu.

Van Gaal, amekua katika minong’ono ya kutimuliwa kazi mwishoni mwa msimu huu, na nafasi yake kuchukuliwa na meneja kutoka nchini Ureno Jose Mourinho, kutokana na matokeo ya kikosi cha Man Utd kutokua mazuri kwa msimu wa pili tangu alipoanza kazi mwaka 2014.

Kamati ya utendaji ya chama cha soka nchini Uholanzi, inaamini Van Gaal anafaa kuwa mkuu wa ufundi katika soka la nchini humo, kutokana na uzoefu alioupata tangu alipoanza shughuli za ukufunzi mwaka 1986 akiwa kama meneja msaidizi wa klabu ya AZ Alkamar.

Kushindwa kufuzu katika fainali za mataifa ya bara la Ulaya za mwaka 2016 (Euro 2016) kumewafanya viongozi wa KNVB kuamini kuna mahala walipokosea, na hakuna dawa ya kurekebisha kosa hilo zaidi ya kumrejesha Van Gaal ambaye alikuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Uholanzi wakati wa fainali za kombe la dunia za mwaka 2014.

Viongozi wa KNVB, wanaamini mipango na mikakati iliyotumiwa na Van Gaal wakati anasaka nafasi ya kucheza fainali za kombe la dunia za mwaka 2014, ataitumia akiwa kama mkurugenzi wa ufundi kwa kusaidina na kocha mkuu wa timu ya taifa.

Van Gaal mwenye umri wa miaka 64, alifanikiwa kukiongoa kikosi cha Uholanzi katika fainali za kombe la dunia za mwaka 2014, kule nchini Brazil na kumaliza kwenye nafasi ya tatu baada ya kuwafunga wenyeji mabao matatu kwa sifuri.

Sunderland Nao Wafanya Maamuzi Magumu Kwa Emmanuel Eboue
Sir Alex Ferguson Atoa Ya Moyoni Kuhusu Leicester City