Kocha kutoka nchini Uganda Abdalah Mubiru amethibitisha kuachana na Mbeya City baada ya timu hiyo kushuka daraja, huku akitaja sababu mbili zilizochangia matokeo hayo akilaani vikali tukio la kupigwa ngumi na mmoja wa viongozi wa Benchi la Ufundi la Mashujaa FC.

Mubiru alisaini kandarasi ya miaka miwili, ambapo kulikuwa na kipengele cha kuongeza mkataba iwapo watabaki ligi kuu na kuvunjika kama timu itashuka daraja na matokeo ndivyo kama ulisikia na kuona.

Mbeya City ilishuka daraja kupitia mchezo wa ‘Play Off’ baada ya kufungwa jumla ya mabao 4-1 dhidi ya Mashujaa ya Championship na kuungana na Polisi Tanzania na Ruvu Shooting zilizoshuka mapema baada ya kumaliza ligi nafasi mbili za mwisho.

Mubiru amesema kutokana na mkataba ulivyokuwa kwa sasa yuko huru, huku akieleza kuwa sababu ya kushuka timu hiyo ni kikosi dhaifu na kwamba alikosa watu aliohitaji akiwamo kipa, beki wa kushoto na straika baada ya Paul Nonga kustaafu.

Pia amesema Mbeya City ilifanyiwa hujuma za wazi kuanzia mchezo wao dhidi ya Young Africans, KMC FC na zile za ‘Play-Off na Mashujaa FC, hali ambayo iliyowapa wakati mgumu na kwamba kwa sasa anakwenda kupumzika kusubiri ofa mpya popote.

Kocha huyo amesema wakati anakwenda mapumziko hakufurahishwa na tukio la kupigwa ngumi na mmoja wa viongozi wa benchi la ufundi la Mashujaa na kwamba haelewi dhamira ilikuwa ni nini.

Amesema anashukuru kwa sasa hali yake inaendelea vyema baada ya matibabu hospitalini akibainisha kuwa kiongozi huyo alimtafuta mara ya kwanza akamkwepa kabla ya kumrudia tena na kumpiga.

Simba SC, Che Fondoh Malone mambo safi
Lungu alaani utawala wa Hichilema kupoka mali zake