Kikosi cha Azam FC kimeendelea kujifua katika mji wa Sousse nchini Tunisia ilipokita kambi ya majuma matatu kwa maandalizi ya msimu mpya lakini kocha mkuu wa timu hiyo, Msenegal Youssouph Dabo amekiri kuwa wameanza kujipata baada ya kujitafuta.
Dabo amesema, kila siku amekuwa akipata picha mpya kutoka kwa mchezaji mmoja mmoja na timu nzima.
“Tumekuwa na vipindi tofauti tukifanya mazoezi ya nguvu na mbinu kwa nyakati tofauti.
“Nafurahi kuona wachezaji wakijituma bila kuchoka na kuhakikisha wanafanya yale tunayowaelekeza. Nawapongeza kwa hilo,” amesema Dabo.
Aidha kocha huyo amezungumzia matunda ya mechi za kirafiki tatu walizocheza Azam FC hadi sasa huko Tunisia wakianza kwa ushindi wa mabao 3-0 mbele ya Al Hilal ya Sudan, ikafuata ile waliyopoteza kwa kufungwa 3-0 na Esperance na kushinda 2-1 mbele ya US Monastir.
“Ni mechi ambazo tunachokiangalia zaidi siyo matokeo bali ni namna gani wachezaji wetu wamepokea na kufanyia kazi kile tulichowaelekeza mazoezini. Kiasi Fulani wamefanya vizuri lakini tunaendelea kuwajenga ili kufanya vizuri zaidi. Kila hatua tunayopiga kuna kitu kinaongezeka.”