Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssoph Dabo, ametamba kukiongoza kikosi chake kufanya vizuri msimu ujao katika michuano ya ndani, kimataifa.
Dabo ametoa kauli hiyo wakati kikosi cha Azam FC kikijipanga kuanza kambi nchini Tunisia kwa muda wa majuma matatu, kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2023/24, mashindano ya kimataifa.
Dabo amesema kabla ya kuondoka nchini aliiongoza timu katika mazoezi ya siku tatu na kugundua kuwa ana timu bora ambayo ikijipanga vyema itatoa upinzani mkali na kufanya vizuri katika mashindano.
“Baada ya mazoezi ya siku tatu yaliyogawanyika katika vipindi vitano, nimeona ni aina gani ya wachezaji nilionao, wakiendelea hivi Azam itafanya vizuri msimu ujao,” amesema Dabo.
Kocha huyo amesema ana muda mrefu wa kuiandaa timu, kuiboresha kisha kuiongoza katika mashindano na kuanza kuhesabu mafanikio ya msimu huo.
Azam FC iliondoka nchini Jumapili (Julai 07) ikiwa na wachezaji wapya wanne ambao ni mzawa, Feisal Salum, Djibril Sillah (Gambia) na mshambuliaji Alassane Diao na Cheikh Tidiane Sidibe (Senegal).