Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssouph Dabo ameeleza sababu ya kumchezesha pembeni nyota wa timu hiyo Msenegali, Alassane Diao katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji uliopigwa mwanzoni mwa juma hili na kumalizika kwa suluhu.
Nyota huyo ambaye kwa kawaida hucheza mshambuliaji wa kati alianzishwa pembeni huku Dabo akieleza sababu kubwa ya kumchezesha nafasi hiyo nyota huyo ni kutokana na wapinzani wao kujaza viungo wengi katikati.
“Baada ya kuona wapinzani wetu wamejaza viungo wengi eneo la katikati basi ilibidi kumuweka acheze pembeni kwa lengo la kuwasumbua ili kutengeneza mianya itakayotumiwa na wengine ili kutengeneza nafasi,” amesema.
Aidha Dabo ameongeza baada ya kucheza michezo mitatu mfululizo nyumbani amefurahishwa na ari iliyoonyeshwa na wachezaji wa timu hiyo ugenini huku akieleza licha ya kutoshinda ila mwelekeo ni mzuri huko mbeleni.
“Kwa sasa tunaelekeza nguvu zetu katika mchezo na Coastal Union ambao utakuwa ni mgumu na wa kiushindani pia kama huu uliopita na Dodoma lakini malengo yetu ni kuhakikisha hatupotezi hizi pointi kirahisi,” amesema.
Suluhu hiyo ni ya kwanza kwa Azam msimu huu katika Ligi Kuu Bara baada ya kuanza vyema kwenye michezo mitatu ambapo ilianza na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Tabora United, 3-1 na Tanzania Prisons kisha 2-1 na Singida Big Stars.